OnlineMonday, November 25, 2013

MAADHIMISHO YA MIAKA 10 YA MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA: MIAKA 10 YA MAPINDUZI YA MAWASILIANO TANZANIA

 

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inasheherekea maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake huku yakiwemo mafanikio makubwa dhahiri na ya kujivunia katika sekta ya mawasiliano nchini.
 
TCRA ilianzishwa rasmi mnamo tarehe 23 mwezi Novemba mwaka 2013 ili kusimamia Sekta ya Posta na Mawasiliano ya Elektroniki ikkiwemo simu, utangazaji, wavuti pamoja na huduma za Posta. TCRA ilkianzishwa kwa Sheria Na. 12 ya mwaka 2003 iliyoziunganisha Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCC) na Tume ya Utangazaji Tanzania (TBC).


Mkakati mahususi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ni “Kuboresha Maisha ya Watanzania kupitia mfumo makini na thabiti ili kuhakikisha kunakuwa na huduma za mawasiliano kwa wote nchini”. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Tanzania imeshuhudia kukua kwa kasi kwa Sekta ya Mawasiliano. Mamlaka ilianzisha mfumo wa leseni za Muingiliano mnamo tarehe 23 Februari 20005. 

Mfumo huu wa leseni za muingiliano (Convergence Lisensing Framework) umekuwa chachu ya kuongezeka kwa miundombinu mbalimbali ya mawasiliano, huduma mbalimbali kwa kutumia mtandao wa mawasiliano ikiwemo wavuti (internet) na utangazaji.

Makampuni ya simu yameongezeka kutoka kampuni moja ya simu TCRA ilivyoanzishwa mwaka 2003 hadi kufikia makampuni saba (7) yenye wateja wenye laini za simu takribani milioni 28 kulinganisha na idadi iliyokuwepo miaka kumi iliyopita. Huduma za simu za mkononi zimebadilisha maisha ya Watanzania kutokana na huduma mbalimbali zinazopatikana kupitia simu za mkononi. Kuanzia huduma za kutuma fedha kupitia simu, malipo ya Ankara mbalimbali na huduma nyingine nyingi zilizobadilisha maisha na uchumi wa wananchi wa taifa hili. 

Sekta ndogo ya Posta nayo haijabaki nyuma kwani kumekuwepo na ongezeko la watoa huduma kutoka mmoja hadi zaidi ya hamsini wenye kutoa hduma ndani nan je ya Tanzania. Tunatarajia mabadilikjo makubwa kwa watanzania hasa baada yan kukamilika kwa mradi wa anwani mpya za makazi na misimbo ya Posta.


Hali kadhalika, yako mabadiliko makubwa sana katika msekta ndogo ya utangazaji. Kutoka nchi yetu kuwa na Radio moja hadi Zaidi ya redio 85. Aidha kutokuwepo kwa Kituo cha Utangazaji wa Runinga hadi vituo vya utangazaji vipatavyo 26. Watumiaji wa wavuti (intanet wameongezeka kutoka watumiaji million moja hadi takribani milioni 8 na ushee. Sekta ya Mawasiliano imekuwa chimbuko la maendeleo ya nchi kwa kutoa ajira kwa watanzania wengi na hali kadhalika kuongeza mapata ya serekali kwa tozo na kodi mbalimbali zinazotolewa katika sekta.. 


Mamlaka ya Mawasiliano imeshinda tuzo mbalimbali katika masuala ya Udhibiti na Usimamizi Bora wa Huduma za mawasiliano nchini katika kipindi cha kuweko kwake miaka kumi iliyopita. Nchi mbalimbali zimekuja Tanzania kujifunza udhibiti na usumamizi wa masuala nyeti ya mawasiliano kama vile masuala ya uhamaji kuelekea mfumo mpya wa utangazaji wa dijitali, Mifumo ya uanzishwaji wa anwani za makazi na misimbo ya posta, Usimamizi mzuri wa masafa na namba za mawasiliano na mambo mengine mengi. 


MATUKIO MBALIMBALI KATIKA MAADHIMISHO TANGU 25 – 29 NOVEMBER 2013

Katika kusheherekea miaka kumi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, kutakuwa na maadhimisho ya wiki nzima yenye matukio mbalimbali. Tukianzia na mkutano huu na waandishi wa habari uliokusudia kutoa taarifa kwenu na kwa wananchi kuhusu maadhimisho haya, kutakuwa na matukio kadha wa kadha kuelekea kilele cha sherehe za maadhimisho yanayotarajiwa kufanyika tarehe 29 Novemba 2013.Maadhimisho haya yanafanika chini ya kauli mbiu ya; Miaka 10 ya TCRA: Miaka Kumi ya Mapinduzi Katika Sekta ya Mawasiliano


Kesho tarehe 26 Novemba 2013 kutakuwa na tukio maalumu kwa wafanyakazi wa mamlaka ambapo wale waliokuwepo tangu wakati wa kuanzishwa kwa TCRA watatunukiwa vyeti pamoja na zawadi mbalimbali kutambua mchango wao kwa taasisi.


Aidha siku ya tarehe 27 Novemba 2013; kutakua na sherehe ya kutoa udhamini kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vya elimu ya juu wanaochukua masomo ya mawasiliano, sayansi na teknolojia. TCRA kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo imekuwa ikitoa udhaminim katika masomo hayo kwa wanafunzi mahiri kwa nia ya kukuza weledi na kuboresha utumishi katika sekta ya mawasiliano chini ya kinachoitwa “TCRA ICT SCHOLARSHIPS” kwa wanafunzi wa digrii ya kwanza, digrii za Uzamili na Uzamivu.

 
Kuanzia tarehe 27 – 29 Novemba, kutakuwa na maonesho maalumu katika viwanja vya ukumbi wa mikutano wa Mlimani City ambapo watoa huduma mbalimbali za mawasiliano nchini wataonesha mafanikio yao na huduma wanazotoa kwa wananchi. Napenda kuchukua fursa hii kuwasihi waandishi wa habari kuhudhuria maonesho haya ili kujifunza na kutumia fursa hiyo kuelimisha jamii ya watanzania kuhusu huduma mbalimbali za mawasiliano zinazopatikana nchini ili wachangamkie fursa.


Hali kadhalika, katika maadhimisho haya, TCRA imeandaa washa maalumu ya siku mbili wa wadau wa mawasiliano kujadili fursa, changamoto pamoja na namna gani kwa pamoja tunavyoweza kufanya mawasiliano kuwa bora Zaidi nchini mwetu. Warsha hiyo itafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City na itafunguliwa rasmi tarehe 28 mwezi huu na Mhe.Dr Mohammed Gharib Billal Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na utaendelea hadi tarehe 29 Novemba 2013. 

 
Wadau mbalimbali wa Mawasiliano kama vile kituo cha Habari cha Tanzania Network Information Centre (tzNIC), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote - (UCSAF), Wamiliki wa Vyombo Vya Habari -(MoAT), na Umoja wa Makampuni ya Simu  (MoAT-Mobile Telephony Companies), Africa Media Group, Agape Associates and TTCL watawasilisha mada mbalimbali.


Vyombo vya Habari vinakaribishwa katika shughuli zote za maadhimisho ya Miaka 10 ya TCRA ili kutoa elimu kwa umma lakini pia kama fursa ya kujionea mafanikio ya sekta ya mawasiliano katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ili kuwawezesha wananchi kufahamu tulikotoka, tunakoenda na fursa zilizoko katika sekta ili kuboresha maisha yao. 

Imetolewa na: 
Mkurugenzi Mkuu 
25th November 2012

Tuesday, November 19, 2013

JAMII PRODUCTION-DAKIKA 90 ZA DUNIA:HATARI YA BUNDUKI ZA KUCHAPISHWA NCHINI MAREKANI

Bunduki ya plastiki iliyotengenezwa kwa mashine ya 3D ikifyatua risasi wakati wa majaribio
Photo credits: Screenshot from ATF Video
Kama tulivyoripoti katika ripoti hii ya Septemba 21, mauaji ya kutumia bunduki ni kati ya matatizo makubwa nchini Marekani.
Lakini pia, uwezo wa nchi hiyo katika teknolojia umesaidia kupunguza madhara ya vifo hivyo kwa kuwezesha kukamatwa kwa silaha kabla hazijafanya madhara.
Hii inajumuisha pia kutumia vifaa maalum vya kugundua vitu vya chuma ambavyo mtu anaweza kuwa ameficha. Hata hivyo, kukua huko kwa teknolijia pia kuna athari katika mapambano dhidi ya uhalifu.
Wiki hii, kitengo kinachojishughulisha na udhibiti wa Pombe, Tumbaku, Bunduki na Milipuko nchini Marekani (ATF) kimetoa ripoti kuhusu athari ama madhara yanayoweza kusababishwa na bastola za plastiki zinazochapishwa katika umbo halisi (3D Guns)

Hii ni sehemu ya ripoti ya Jamii Production kwenye kipindi cha DAKIKA 90 ZA DUNIA kinachorushwa na kituo cha Radio cha Capital FM cha Dar Es Salaam Tanzania kila Jumamosi kuanzia saa moja na nusu asubuhi (7:30 AM).
Bahati Alex (L) Capital Radio Jijini Dar es Salaam na Mubelwa Bandio (R) wa Jamii Production Washington DC
Hii ilikuwa ripoti ya Novemba 16, 2013

Kwa maoni, ushauri, nk usisite kutuandikia jamiiproduction@gmail.com

Monday, November 18, 2013

GOOGLE NA MICROSOFT KUDHIBITI PICHA ZA KUDHALILISHA WATOTOKampuni za Google na Microsoft zinazoongoza duniani kwa mitandao yao kutumika kutafuta taarifa mbalimbali zimekubaliana kuchukua hatua za kuhakikisha inakuwa vigumu kupata picha zinazowadhalilisha watoto katika mitandao.

Maombi kufikia 100,000 yakitafuta picha hizo, hayatapata matokeo yoyote ya utafutaji picha za kudhalilisha watoto na taarifa nyingine zilizo kinyume cha sheria.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, ambaye alitoa wito kwa kampuni hizo kuchukua hatua za kuwanusuru watoto kutokana na udhalilishaji huu, amepongeza hatua hiyo.

Lakini ameonya kuwa lazima hatua hiyo itoe matokeo mazuri, vinginevyo ataleta sheria mpya ya kuyabana makampuni hayo ya mawasiliano.

Mwezi Julai, 2013, Bwana Cameron alizitaka kampuni za Google na Microsoft ambazo kwa pamoja zinachangia asilimia 95% ya utafutaji wa taarifa mbalimbali kwa njia ya mtandao, kuchukua hatua zaidi ili kuzuia watu kupata picha mbaya.

Alisema kwamba wlitakiwa kuhakikisha kuwa maombi yanayotumwa kutafuta taarifa ambazo zinalenga kupata picha chafu, yasitoe majibu yoyote.

Kwa sasa kampuni zote mbili zimeanzisha "programu mpya ya kompyuta" ambayo itazuia utafutaji wa picha zinazowadhalilisha watoto.

Akiandika katika gazeti la Uingereza la Daily Mail, mwenyekiti mtendaji wa Google Eric Schmidt amesema: "Mabadiliko haya yameondoa maombi zaidi ya 100,000 ambayo huenda yalihusishwa na udhalilishaji wa watoto.

"Likiwa jambo muhimu, hivi karibuni tutaweka mabadiliko haya katika zaidi ya lugha 150, hivyo matokeo ya hatua hii kuwa ya dunia nzima."

Ameendelea kueleza kazi ya kuzuia picha za udhalilishaji watoto, kwa kusema:"Sasa tunaonyesha - kutoka mtandao wa Google na mengine, juu ya chumba cha kutolea maombi ya kutafuta taarifa mbalimbali kwa maombi zaidi ya 13,000.

"Maonyo haya yanaonyesha wazi kwamba udhalilishaji wa watoto ni kinyume cha sheria na kutoa ushauri wa mahali pa msaada."

Jumahili, kampuni mbili hizo za Google na Microsoft zitaungana na kampuni nyingine za internet katika ofisi za waziri mkuu wa Uingereza zilizopo Downing Street, kwa ajili ya Kikao cha Usalama wa Internet.
chanzo:BBC

Friday, November 15, 2013

MAMBO MANANE YA KUZINGATIA JUU YA MATUMIZI YA MITANDAO YA JAMII


 

Siku hizi, katika kila watu kumi wanaotumia mtandao, basi angalau watano kati ya hao wanatumia mitandao jamii. Kuna baadhi ya watu wamegeuza mitandao hii kuwa kama ni sehemu ya mawasiliano, ama ya mtu kwa mtu au ya kibiashara. Siku hizi, si kitu cha kushangaza kusikia mtu maarufu au kiongozi fulani atakuwa kwenye Facebook saa fulani kwa ajili ya kujibu maswali ya wananchi / mashabiki wake. Mitandao hii ni kama vile Facebook, Twitter, Jamiiforums nk, hivyo basi, hatuwezi kuepuka ushawishi wa mitandao jamii katika jamii yetu.

Matumizi bora ya mitandao jamii huweza kuleta faida nzuri sana, ila huwa kinyume pale inapotumika sivyo, ama kwa kutokujua ama kwa kuamua. Hivyo leo hii tuangalie mambo kadhaa ya kuepuka unapotumia mitandao jamii.


1. EPUKA KUJIACHA WAZI KWENYE MITANDAO JAMII.Kuna baadhi ya watu wamegeuza mitandao jamii ni dunia yao nyingine kabisa, wao kila kitu wanachokifanya utakiona kwenye mitandao jamii, kala nini, anamchumbia nani, kavaa nguo gani nk. Mitandao jamii ni uigaji (Simulation) ya maisha ya halisi.Tukiwa kwenye maisha halisi, sio watu wote wanaoweza kujua maisha yako kwa undani,kwani kuna vikomo, kuanzia wale mulio nyumba moja, munaofanya kazi pamoja nk.


Ingawa kwenye mitandao jamii wengi wanaweza kuchunga kwa kutumia michungo ya ufaragha (Privacy setting) lakini si wote wanaojua hilo, pia tumeona mamia ya akaunti za watu zikivamiwa na wavamizi wa mtandao (Hackers) na kuweka hadharani taarifa zao nyingi. Hivyo epuka kuweza kila kitu kwenye mitandao jamii, kula na kikomo na pia anza kuchunga marafiki zako juu ya nani anaweza kuona nini. Unaweza kuangalia Video HAPA jinsi ya kuchunga ufaragha kwenye Facebook.


2. JICHUNGE KWENYE UTUMAJI.
 
Je ushawahi kusikia mtaani wanasema jamaa ana gubu (anaongea sana?), kwenye mitandao jamii pia kuna watu wana gubu, wanachonga sanasana. Hawa ni wale watu ambao kila dakika wametuma kitu kipya, hii sio tu hufanya kupoteza mvuto kwa wanaokufuatilia, bali pia umuhimu wa makala zako hupungua. Binafsi huondoa watu aina hii kwenye mlisho wa maboresho (activities feeds) bila hata kujiuliza.

Hivyo, ili kuepuka kutengwa au kuonekana unachonga sana, chunga idadi ya maboresho unayotuma kwa siku.


3.EPUKA KUTUMA MAKALA ZA NGONO, DINI AU SIASA KAMA WEWE SI MUHUSIKA.


Hivi ni vitu ambavyo huathiri watu wengi sana, chukulia mfano wewe ni rafiki wa bwana X, unafungua Facebook au Twitter yako unakutana na picha ya ngono imejaa kwenye mlisho wa maboresho toka kwa rafiki yako. Ukweli ni kuwa utajisikia vibaya mno ama kama na wewe ni wa aina hiyo. Hii pia ni sawa na kwa mambo ya dini na siasa.


Tanzania ikiwa ni nchi isiyo na dini, ila watu wake wamechanganyika mnomno, kwenye kila marafiki zako wawili, kuna mmoja ni wa dini nyingine, hivyo epuka kutuma makala za dini zinazoudhi, zenye kebehi au kuudhi wengine. Jaribu kuwa mtu ambaye utaweza kuishi na watu wote. Mfano huu pia tuuchukue kule uraiani, kuna baadhi ya watu hukimbiwa, hivyo chukua tahadhari kabla ya kukimbiwa.

4. USIHAMISHIE HASIRA ZAKO KWENYE MITANDAO JAMII.
Kuna baadhi ya watu, wakishauziwa nyumbani, hasira zinaishia kwnye mitandao jamii,amini usiamini, mitandao jamii haiwezi kukusaidia kutuliza hasira zako zaidi ya kukupotezea muda na kujidhalilisha. Ni sawa na yule mtu mwenye ugomvi na mke / mume wake halafu anapita kila nyumba kutangazia mapungufu ya mwenza wake, jamii nzima inajua, siku mutakaporudiana, watu wote washajua mapungufu ya mwenza wako, je utafuta toka kwenye vichwa vyao? Kwenye mitandao jamii vilevile, kuna baadhi ya watu kuhifadhi kila unachotuma na siku ya siku watatumia kuja kukashambulia. Kaa mbali na mitandao jamii kama unaona hauwezi kuchunga mhemuko (emotion) wako.


5.SIYO KILA MTU LAZIMA AWE RAFIKI YAKO.


Chukulia mfano mitaani tunamoishi, kuna watu wa aina mbalimbali, na siyo kila mtu ni rafiki yako, kuna baadhi ya watu hata hautaki kuwasogelea kutokana na tabia zao, hii ni sawa kwenye mitandao jamii. Epuka kukubali maombi ya urafiki toka kwa kila mtu, haswaa ambao hauwafahamu. Marafiki sio tu huweza kutumika kujenga taswira yako, bali kuna baadhi ya marafiki si marafiki, hivyo chunga marafiki zako la sivyo ipo siku utakuja kujuta.

6 . UHIFADHI WA HISTORIA
Uhifadhi wa historia - Ni vizuri kujua kila unachofanya kwenye mitandao ya kijamii haswa kutumia account yako kama ni email au nini kinahifadhiwa sehemu , kama umekashifu mtu , kama umejiunga kwenye vikundi vya kiharamia au kama umetafuta kitu kinachohusiana na ugaidi au kutengeneza mabomu yote hii huwa inahifadhiwa usishangae siku moja ukagongewa mlango kuonyeshwa kile ulichokuwa unafanya na rumande moja kwa moja .

7.KUJIUNGA KWENYE VIKUNDI AU UKURASA
Kuna watu wanapenda kulike kurasa za facebook za watu , vikundi na nyingine nyingi bila kufuatilia vizuri , unaweza kulike leo kwa nia nzuri tu kwa sababu ana habari nzuri baada ya siku kadhaa kupata watu wengi mtu huyu au kikundi kinaweza kuanza kuweka mambo yake yaliyojificha na inaweza kukuweka katika nafasi mbaya kama ni katika familia , kazini , utumishi wa umma au sehemu za harakati ingawa una uhuru wa kuchagua .

8 - KUHUSU TABIA ZA MTU 
Kutumia mitandao ya kijamii kama facebook na myingine unaweza kujua tabia za mtu , vile anavyopenda , rafiki zake , wanafamilia wake , mke wake , mume , watoto , wafanyakazi wenzake na tabia nyingine za ajabu au nzuri na vile vile kwenye tekinologia ya mawasiliano siku hizi kuna mfumo wa tabia za watu kujulikana - kile ambacho unapenda kutafuta au kuongelea ndicho utakachokuta kwenye email yako kama tangazo au kurasa yako ya facebook kama TAG 
Hayo ni mambo muhimu kwa ajili ya afya ya utumiaji wa mitandao jamii, usisahau kulike Kurasa yetu ya Facebook kwa makala mbalimbali za IT kila wiki https://www.facebook.com/dudumizi
  

Imeandikwa na Yona Msuya toka tovuti ya dudumizi na Yona Maro wa wanabidii forum

TCRA - WANAOVUJISHA MAWASILIANO YA WATU WASHITAKIWE

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kampuni za simu za mikononi, zimewataka wateja watakaokumbwa na tatizo la kuvujishwa kwa taarifa za simu, kuripoti kwenye vyombo vya dola ili hatua zichukuliwe.

Aidha imeelezwa kuwa ingawa kumekuwa na mashine za kuzuia taarifa za siri za simu za mikononi kutovuja, baadhi ya wafanyakazi wa kampuni za simu wasio waaminifu wamekuwa wakihujumu wateja kinyume cha sheria kwa kuchezea teknolojia isivyopaswa.

Hadhari hiyo imekuja kukiwa na wimbi la matumizi mabaya ya simu za mkononi nchini Tanzania, ikiwemo matumizi ya teknolojia kutoa 
hadharani mawasiliano ya siri ya watu.

Miongoni mwa matukio ya hivi karibuni, ni taarifa zilizoanikwa kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Kabwe Zitto, zikionesha mawasiliano ya siri anayodaiwa kufanya na watu mbalimbali yakidaiwa kuwa ni ya kuhujumu chama chake.

Matumizi mengine ni aliyodai kufanyiwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema, ambapo pamoja na namba za simu kadhaa kudai zinamtumia ujumbe wa matusi, pia alidai upo ujumbe wa matusi unaotumwa kwa watu na namba inayojitokeza ikionesha ni ya mbunge huyo suala alilosema juzi limemchafua kisiasa na kijamii.

Akizungumza jana na mwandishi juu ya matukio hayo, Meneja Uhusiano wa TCRA, Innocent Mungy, alisema kampuni za simu zinaongozwa kwa mujibu wa sheria hivyo hakuna itakayokubali kutoa taarifa za siri za mteja kwa kuwa ni hatari kwao.

Sheria husika ni ile ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010 inayotoa kinga kwa mteja.

“Ninachojua ambacho kinaweza kuonekana na kupatikana kutoka katika kampuni hizo tena kama zikiombwa na Polisi ama vyombo vya usalama kufanya hivyo kwa kulinda usalama wa taifa, ni kuelezwa siku fulani uliwasiliana na nani na saa ngapi na kampuni zinaweza kuchapa taarifa hiyo na kuitoa bila kueleza kilichozungumzwa wazi wazi,” alisema Mungy.

Mungy alisema kampuni za simu zina utaratibu wa mafundi wake kuingia chumba cha kuhifadhi taarifa za siri, na ikiwa mtu ana uhakika namba ya kampuni fulani imetumiwa visivyo, anapaswa kutoa taarifa Polisi ili hatua zichukuliwe kwa kuwa hilo ni kosa la uhalifu wa mtandaoni.

“Naomba ieleweke kwamba haiwezekani mtu asikilize maongezi ya mtu na mtu, ama kusoma ujumbe mfupi wa simu za mkononi, ingekuwa hivyo wafanyabiashara wakubwa wasingefanya biashara wala taarifa za ulinzi na usalama wa nchi zisingekuwa siri leo, watu waondoe hofu na ikiwa mtu katendewa hivyo kweli, aende Polisi kupata haki yake,” alisisitiza Mungy.

Ofisa Mawasiliano wa Kampuni ya simu ya Zantel, Monica Ekelege akizungumzia suala hilo, alisema mafundi katika kampuni za simu wana uwezo wa kuona mawasiliano ya mtu na mtu ikiwa wanatafuta kitu na kujua namba ya mtu, lakini hawawezi kutoa mawasiliano hayo kwa kuwa kampuni nyingi zina mashine ya kuzuia siri.

“Huu ni uhalifu kama uhalifu mwingine, mtu anaweza akachokonoa chokonoa na kuibuka na njia nyingine ya kuvujisha taarifa za mtu, huyu akibainika, sheria haimwachi lakini kwanza kwa kuwa sisi tunafanyakazi chini ya sheria inayomlinda mteja na siri zake, ana mamlaka ya kutushitaki lakini lazima awe na uthibitisho na kuanzia Polisi,” alisema Ekelege.

Ekelege alisema uhalifu mwingi wa simu wanaoufanya watu, wanatumia udhaifu wa baadhi ya mawakala waliozembea kutumia vielelezo stahiki katika kusajili namba za simu, na sasa baadhi wanatumia mwanya huo kufanya uhalifu.

Kuhusu watu wanaotumia simu kutuma ujumbe wa matusi au kufanya uhalifu mwingine kama vile utapeli, Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando, alisema mara nyingi wanaofanya vitendo hivyo ni wenye simu ambazo hazijasajiliwa kwa kufuata utaratibu unaopaswa.

Alisisitiza waathirika wa vitendo hivyo kutoa taarifa Polisi na kampuni yao itatoa ushirikiano kubaini wahusika ili hatua zichukuliwe.

Saturday, November 2, 2013

NAMNA UNAVYOWEZA KUFUTA TAARIFA ZAKO KWENYE MITANDAO NA TOVUTI MBALIMBALI

Huenda umekuwa ukitumia intaneti na hasa mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter, Google+,LinkedIn na mingine mingi na umeona unataka kujiondoa kabisa ama kuondoa kabisa taarifa zako zisiendelee kuonekana katika mitandao hiyo kuna njia chache za kuweza kufuata.
How to Erase Yourself From the Internet
Hii ni njia ya kufuta taarifa zako kwenye facebook

Facebook

Facebook imeweka njia ambayo iko wazi kuonekana kwa kila mtumiaji ambaye anataka kujiondoa kwenye mtandao huo nayo ni kusitisha yaani kudeactivate ambayo unaweza kuipata kwenye  Account Settings > Security > Deactivate your account. Usidanganyike siyo kwamba inaondoa taarifa zako bali inazitunza taarifa zako ili unapobadilisha uamuzi wa kurudi tena uzipate taarifa hizo. 

Kama unataka kweli kuondoa taarifa zako basi unahitaji kulogin kwenye wasifu wako kisha bofya  Delete My Account na baada ya hapo bofya kibox cha bluu hapo utakuwa umeondoa kila kitu kwenye mtandao wa kijamii wa facebook na huwezi kuzirudisha tena japo itabidi usubiri baada ya siku 40 zitakuwa zimeondolewa kabisa .

Japo kabla ya kufanya inakupasa uhamishe taarifa zako na mambo yote kwenye tarakirishi yako kwa kufanya hatua zifuatazo Account Settings > General > Download a copy of your Facebook Data > Start My Archive.

Twitter

Kama ilivyo kwenye facebook ,katika mtandao wa  Twitter deactivate ina maanisha ondoa ama futa,ni rahisi sana nenda  Account Settings > Deactivate my account > Okay, fine, deactivate account. na hapo weka neno lako la siri imemalizika.
Twitter nayo hutunza kumbukumbu zako kwa siku 30 ikiwa utabadilisha uamuzi utazikuta taarifa zako,usipofanya hivyo baada ya muda huo zitakuwa zimeondolewa 

 How to Erase Yourself From the Internet
 Hiyo ni baadhi ya mifano ya kuondoa taarifa zako katika tovuti ya accountkiller.com inatoa maelezo ya mbinu mbalimbali za kufuta taarifa zako katika mitandao mbalimbali ya kijamii 

Friday, November 1, 2013

KARIBIA NUSU YA MAPATO YA MATANGAZO YA BIASHARA YA FACEBOOK YANATOKA KATIKA SIMU ZA MIKONONI


Facebook imeeleza juma hili kuwa ilipata mapato ya jumla ya dola za kimarekani bilioni 1.8 kutokana na matangazo ya biashara, ambapo asilimia 44 kati ya asilimia 49 ya matangazo yanatoka katika simu za mikononi katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2013.

Katika robo ya tatu mwaka 2012 facebook ilipata asilimia 14 tu kutokana na matangazo ya kwenye simu za mikononi.

Takwimu zinaonesha kuwa watu milioni 874 wenye simu za mkononi wanatumia mtandao wa facebook kwa mwezi,na kuna ongezeko la asilimia 45 mwaka hadi mwaka na kubaki kuwa mtandao wa kijamii unaotumiwa na watu wengi ambapo kila mwezi hutumiwa na zaidi ya watu milioni 1.19 duniani.