OnlineWednesday, July 31, 2013

KAMPENI YA KUHAMASISHA MATUMIZI MAZURI YA MAWASILIANO


KAMPENI YA KUHAMASISHA MATUMIZI MAZURI YA MAWASILIANO

Siku za hivi karibuni, ongezeko la huduma za mawasiliano nchini limekuwa kwa kasi sana. Huduma za mawasiliano nchini katika kipindi kifupi zimekuwa sana na kuwafikia Watanzania wengi zaidi. Kutoka laini za simu za mkononi milioni tatu tu mwaka 2000 hadi kufikia laini 28,000,000.

Watanzania walio wengi hivi sasa wanafaidika kwa huduma za mawasiliano, yakiwemo mawasiliano ya simu za mikononi, utangazaji. Vile vile huduma za ziada kama kutuma na kupokea fedha kwa kutumia mitandao na simu za mkononi zimeongezeka maradufu. Wananchi wengi wanapata huduma za kibenki kwa kutumia simu zao, wanawasiliana kwa kutumia simu zao kupitia sauti, SMS na kadhalika.

Hali kadhalika kumekuwa na ongezeko la matumizi ya intaneti kwa watanzania walio wengi kutoka watumiaji laki tatu miaka mitatu iliyopita hadi watumiaji milioni 7.6 kwa takwimu za hivi karibuni. Wengi wa watumiaji wa intaneti matumizi yao ni katika kujifunza na kujielimisha pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, BBM, LinkedIn na blog mbalimbali zinazotoa habari mbalimbali zikiwemo za kimaendeleo, burudani pamoja na michezo.

Matumizi haya ya intaneti yamewanufaisha watanzaia walio wengi kwani ni fursa murua ya kujifunza kupitia mitandao hiyo ya kijamii kwa kupata habari mpya, kujifunza na kuelimishana kuhusu shughuli za maendeleo na kuleta amani miongoni mwa watanzania.

Hata hivyo pamoja na maendeleo haya, kumekuwepo na baadhi ya watu wachache wanaotumia mawasiliano ya simu, mitandao ya kijamii, redio, TV na mawasiliano mengine kwa lengo la kuvuruga amani, kuchocheo vurugu, kuchonganisha watu, kusababisha ugomvi, kuwaumiza wengine kwa mambo yasiyo na ukweli, kupotosha jamii na hata kuvuruga maendeleo kwa ujumla.
 
Julai 31,2013 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inazindua kampeni ya kuelimisha umma kuhusu matumizi mazuri ya mawasiliano na inawatahadharisha wananchi kwamba kutumia mawasiliano vibaya kama ilivyoainishwa katika sheria ya Mawasiliano ya Kielectroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 ni makosa. Katika kampeni hii, Mamlaka inakusudia kuwasihi wananchi kuhakikisha wanatumia mawasiliano vizuri ili kudumisha amani, mshikamano na upendo miongoni mwa watanzania.

Katika uzinduzi huu, Mamlaka imewaalika baadhi ya watumiaji mahiri wa mitandao ya kijamii ambao wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watanzania walio wengi wanafaidika na mawasiliano. Miongoni mwao wako wamiliki wa blog mbalimbali, wasimamizi wa makundi mbalimbali katika mtandao wa FB na mengineyo. Nia ya Mamlaka ni kuomba ushirikiano kwao ili waweze kushiriki katika kampeni hii na kuwahamasisha mashabiki wao kutumia vizuri mitandao ya kijamii ili kunufaisha Taifa letu kwa matumizi mazuri.

Watumiaji wa simu za mkononi na wananchi wote wanashauriwa kuunga mkono juhudi zinazofanyika ili kufanikisha kampeni hii kwa ajili ya kudumisha na kuendeleza amani na usalama na kuharakisha maendeleo ya sekta ya Mawasiliano inaendelea kuchangia uchumi wa Taifa na kuiweka Tanzania katika mazingira mazuri zaidi kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Tunawasihi wananchi na watumiaji wa huduma za mawasiliano kuwa wakipokea ujumbe wowote wa kueneza chuki, unaopelekea kuvuruga amani, uchochezi na kuvuruga amani, toa taarifa kwa vyombo husika, kisha futa ujumbe huo. Usiueneze kwa wengine kwani utakuwa sehemu ya uhalifu.

Imetolewa na:

MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
31 Julai 2013

Saturday, July 27, 2013

KALAMU YA KUGUNDUA MAKOSA UNAPOANDIKA YAGUNDULIWA 

 Na Brown Nyanza
Wanasayansi wawili katika nchi ya Ujerumani wamegundua kalamu inayotoa alama pindi mwandishi anapokosea herufi “spelling error.” Kalamu hiyo imepewa jina la Lernstift neno la kijerumani linalomaanisha learning pen, Yaani kalamu ya kusomea ama kujifunzia

 Katika mahojiano maalumu katika kituo cha CNN, Mmoja ya Wanasayansi hao alisema wazo la kalamu hiyo limekuja baada ya kuona mke wake akikasirika mara kwa mara pindi anapomuona mtoto wao akihangaika kwa kukosea  herufi kila mara wakati wa kufanya mazoezi ya nyumbani (homework), 

Ndipo akasema kwa hasira “kwanini kusiwe na peni inayotoa alama fulani pindi mtoto anapokosea herufi wakati wa kuandika.” Ndipo mawazo ya mumewe yakaenda mbali zaidi na kufikiria kuteneneza peni hiyo iliyoleta gumzo kubwa duniani. 

Kalamu  hiyo hutoa alama kwa kutetemeka “vibration” pindi unapokosea herufi wakati wa kuandika.

Kwa sasa kalamu  hiyo inagundua lugha mbili tuu, kingereza na kijerumani, pia unaweza kuunganisha na Smartphone yako, tabiti au computer na kuona kitu unachokiandika katika karakasi.

Chanzo: CNN

GOOGLE PLAY YAONGOZA KWA KUWA NA PROGRAM TUMISHI NYINGI


 
Na:Brown Nyanza
Kampuni ya Google mapema juma lilopita katika tukio la kuzindua kifaa chake cha chromecast  na tabiti yake mpya ya Nexus 7, Imetoa takwimu ambazo zinaiweka Hifadhi yake ya program tumishi iitwayo  “Google play” kuwa ndio  inayoongoza kwa kuwa na program tumishi nyingi duniani ikiiacha nyuma hifadhi nyingine ya progam tumishi inayomilikuwa na Apple iitwayo Apples Store. 

“Google play” Ina jumla ya program tumishi (applications) zaidi ya milioni moja, Wakati Apple’s App store ina jumla ya program tumishi laki tisa. Programu tumishi hizo ni pamoja na vitabu vya mtandao (digital books), muziki, michezo ya tarakirishi (games), vipindi vya televisheni na mengineyo mengi.
Chanzo:(www. gsmarena.com)

MATUMIZI MABAYA YA MAWASILIANO NA UDANGANYIFU KATIKA USAJILI WA NAMBA ZA SIMU ZA MKONONI TANZANIA NI KOSA LA JINAI

1.  Huduma za mawasiliano nchini katika kipindi cha miaka kumi iliyopita zimekuwa sana na kuwafikia watu wengi zaidi. Ni ukweli usiopingika kuwa watanzania wengi hivi sasa wanafaidika kwa huduma za mawasiliano, hususani katika mawasiliano ya simu za mikononi, utangazaji, intaneti na huduma za ziada kama kutuma na kupokea fedha kwa kutumia mitandao na simu za mkononi. Wananchi wengi wanapata huduma za kibenki kwa kutumia simu zao, wanawasiliana kwa kutumia simu zao kupitia sauti, SMS na kadhalika.
2.    Aidha kumekuwa na ongezeko la matumizi ya intaneti kwa watanzania walio wengi hususani matumizi ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook, twitter, BBM, LinkedIn na blog mbalimbali. Matumizi haya yamewanufaisha watanzaia kwani ni fursa murua ya kujifunza kupitia mitandao hiyo ya kijamii kwa kupata habari mpya, kujifunza na kuelimishana kuhusu shughuli za maendeleo na kuleta amani miongoni mwa watanzania.

3.    Pamoja na maendeleo haya chanya kwa nchi yetu, kumekuwepo na baadhi ya watu wachache wanaotumia mawasiliano ya simu, mitandao ya kijamii, redio, TV na mawasiliano mengine kwa lengo la 

kuvuruga amani, kuchocheo ugomvi, kuchonganisha watu, kusababisha ugomvi, kuwaumiza wengine kwa mambo yasiyo na ukweli, kupotosha jamii na hata kuvuruga maendeleo kwa ujumla.
4.    Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inawatahadharisha wananchi kwamba ni kosa la jinai kutumia mawasiliano vibaya kama ilivyoainishwa katika sheria ya Mawasiliano ya Kielectroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010. Wananchi wanashauriwa kuhakikisha wanatumia mawasiliano vizuri na kuhakikisha tunadumisha amani na upendo miongoni mwa watanzania.

5.    Aidha mamlaka inapenda kuwakumbusha wananchi kuwa kusajili laini yako ya simu, kwa kutumia utambulisho wa udanganyifu pia ni kosa la jinai. Mtumiaji wa huduma za mawasiliano unatakiwa kwenda kwa mtoa huduma au wakala wake ukiwa na kitambulisho sahihi chenye picha yako na kutoa taarifa sahihi. Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010, kifungu cha 131, kimeainisha kuwa ni kosa la jinai kutumia au kuwezesha kutumika namba ya simu isiyosajiliwa. Adhabu ya faini ya shilingi laki tano (Tshs 500,000.00) au kifungo cha miezi mitatu itatolewa kwa yeyote atakayekiuka sheria hii.

6.    Kuanzia tarehe 1 Juni 2013 saa sita usiku, laini zote za simu ambazo hazijaanza kutumika zilifungwa (locked) na haziruhusiwi kutumika hadi mtumiaji atakapoisajili laini yake mpya kwa watoa huduma. Kama kuna mwananchi atakaenunua laini, na kuweza kuitumia bila ya kuisajili, anaombwa kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).   

7.    Watumiaji wote wa simu za mkononi ambao hawakuwa wamesajili namba zao za simu wafanye hivyo mara moja. Ifahamike kwamba ilipofika tarehe 10 Julai 2013 saa sita usiku, laini za simu ambazo zilikuwa zinatumika na zilikuwa bado hazijasajiliwa hadi wakati huo, zilifungwa. Kufungua laini iliyofungwa, mtumiaji atapaswa kwenda kwenye ofisi ya mtoa huduma wake au wakala wake kusajili upya na kuthibitishwa ili laini yake ifunguliwe.

8.    Watumiaji wa simu za mkononi na wananchi wanashauriwa kuunga mkono juhudi zinazofanyika ili kufanikisha usajili wa namba za simu kwa ajili ya kudumisha na kuendeleza amani na usalama na kuharakisha maendeleo ya sekta na ya Taifa kwa ujumla.

9.    Faida za kusajili laini ya simu ni nyingi zikiwemo usalama katika huduma za kutuma na kupokea pesa kwa mitandao ya simu. Kununua na kulipia gharama mbalimbali zikiwemo za bili za umeme, maji, na ushuru na pia kusaidia upelelezi iwapo kuna matumizi mabaya ya simu.

10.  Mamlaka inapenda kuukumbusha umma kuwa ni kosa la jinai:

a)   Kuuza laini za simu kama wewe si wakala wa mtoa huduma: Iwapo mtu atakamatwa na kutiwa hatiani akiuza laini za simu ikiwa yeye si wakala wa kampuni ya simu atahukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni saba au kufungwa jela miaka miwili au adhabu zote mbili kwa pamoja.

b)   Kutumia simu isiyosajiliwa: Mtu yeyote anayetumia simu isiyosajiliwa anatenda kosa la jinai na akitiwa hatiani atahukumiwa kulipa faini isiyozidi shilingi laki tano, au kifungo cha miezi mitatu jela.

c)    Kutoa taarifa za uongo wakati wa kusajili namba ya simu: Mtu yeyote atakayetoa taarifa za uongo akijua kuwa taarifa hizo si za kweli anatenda kosa la jinai na akitiwa hatiani atahukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni tatu au kifungo cha miezi kumi na miwili au adhabu zote kwa pamoja.

d)   Kumsaidia mtu mwingine atende kosa kwa mujibu wa sheria za mawasiliano naye anatenda kosa na akitiwa hatiani atahukumiwa kulipa faini isiyozidi shilingi milioni tatu au kufungwa jela miezi kumi na miwili au adhabu zote mbili kwa pamoja.

e)   Kutumia njia yeyote ya mawasiliano kuvuruga amani, kugombanisha watu, kufanya uchochezi wa kidini au kisiasa, kueneza chuki, kusambaza uongo na kuleta vurugu katika jamii ni kosa la jinai na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaobanika kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.

f)    Mwananchi ukipokea ujumbe wowote wa kueneza chuki, unaopelekea kuvuruga amani, uchochezi na kuvuruga amani, toa taarifa kwa vyombo husika, kasha futa ujumbe huo. Usiueneze kwa wengine kwani utakuwa sehemu ya uhalifu.

Imetolewa na:


MSEMAJI MAMLAKA YA MAWASILIANO
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

 26 July 2013

Wednesday, July 24, 2013

RAIS WA TANZANIA JAKAYA KIKWETE ATOA MAELEKEZO KUHUSU KODI YA LAINI ZA SIMU ZA MIKONONI.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja na maofisa waandamizi wa Wizara ya pamoja na wajumbe wa Chama cha Makampuni ya Simu za mkononi alipokutana nao kwa mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Julai 23, 2013.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameagiza Wizara za Serikali zinahusika na kodi na mawasiliano pamoja na makampuni ya simu za mikononi nchini Tanzania kukutana mara moja kutafuta jinsi gani ya kumaliza mvutano wa kodi mpya ya kadi(laini) za simu hizo za mikononi.

Rais kikwete ametoa maelekezo hayo jioni ya Jumanne, Julai 23, 2013 wakati alipokutana na viongozi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na wawakilishi wa makampuni ya simu ya TTCL, Airtel, Vodacom, Tigo na Zantel katika kikao cha pamoja kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Rais Kikwete amesema kuwa lengo kuu la mkutano huo wa pamoja kati ya Wizara hizo za Serikali na makampuni ya simu yawe ya kupendekeza jinsi gani ya kuziba pengo la Sh. Bilioni 178 ambazo zitapotea katika Bajeti iwapo kodi hiyo kwa kadi za kuongelea za simu za mikononi italazimika kufutwa na Serikali kupitia marekebisho kwenye Muswada wa Fedha wa Bajeti ya Mwaka 2013/2014.

Rais Kikwete amewaambia wawakilishi wa pande hizo mbili kuwa huwezi tena kuifuta moja kwa moja kodi hiyo bila kutafuta njia nyingine za kupata fedha za kujaza pengo hilo la Sh. Bilioni 178 ambazo tayari Bunge limezipangia matumizi.
“Nawaombeni kaeni pamoja, wekeni bongo zenu pamoja, wekeni akili yenu pamoja tutafute namna gani tunaweza kujaza pengo hili la Sh. Bilioni 178 endapo tutakubaliana kuwa kodi hii inawabebesha wananchi mzigo mzito na kuwa pengine menejimenti ya kodi yenyewe ni ngumu,” Rais Kikwete amewaambia wawakilisho hao.

Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014, Serikali imeweka kodi ya Sh. 1,000/= kwa mwezi kwa kila mtumiaji simu kwa ajili ya kufanya mawasiliano kwa kutumia simu ya mkononi.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu.

Dar es Salaam.

23 Julai, 2013
Chanzo:Jestina.com

Monday, July 22, 2013

FULSA TOKA MOZILLA KWA WANATEKNOHAMA ANGALIA VIDEO HII

SIMU NA EMAIL ZA KUTUMA MALALAMIKO KWA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA TANZANIA

ILI kuboresha utoaji huduma kwa umma hivi karibuni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeanzisha utaratibu wa kupokea malalamiko na taarifa kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani.

Utaratibu huu mpya unatarajia kupunguza usumbufu na gharama kwa walalamikaji, hususan watokao pembezoni mwa nchi katika kuwasilisha malalamiko yao ofisi za Tume na kupata mrejesho. Itakumbukwa kuwa hapo awali baadhi ya wananchi walilazimika kuacha shughuli zao za kiuchumi na kusafiri hadi zilipo ofisi za Tume ili kupata huduma.


Vilevile utaratibu huu utaharakisha mawasiliano kati ya Tume na walalamikaji kwa upande mmoja na kati ya Tume na walalamikiwa, ukilinganisha na njia iliyokuwa ikitumika awali ya barua ya posta ambayo ilikuwa ikichukua muda mrefu na kukabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo kupotea kwa barua na wananchi wengi kutokuwa na anuani za posta za uhakika.

 
Kwa utaratibu huu mpya mtu anaweza kufungua malalamiko Tume pale ambapo ataona haki zake za msingi
zimevunjwa au misingi ya utawala bora imekiukwa kwa kuandika ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani kwenda namba 0754 460 259, naye atapokea majibu ndani ya muda mfupi.

Utaratibu huu mpya siyo tu unampa uhakika mlalamikaji wa lalamiko lake kufika Tume, bali pia unamwezesha kupata ushauri wa kisheria juu ya lalamiko lake ndani ya muda mfupi.

Aidha, utaratibu huu utaisaidia Tume kupata vidokezo (yaani ‘tips’) kuhusu matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora yanayotokea maeneo mbalimbali ya nchi na hivyo kufanya ufuatiliaji kwa wakati.


Utaratibu huu mpya unatarajia kuongeza idadi ya malalamiko yanayowasilishwa Tume kutoka wastani wa malalamiko 80 hivi sasa hadi 200 kwa Mwezi. Tume imejipanga kikamilifu kuyashughulikia malalamiko yote ndani ya muda mfupi. Hii inatokana na ukweli kwamba hivi sasa Tume inatumia mfumo wa kielektroniki ujulikanao kwa lugha ya kigeni kama “Case Management System,”  katika kushughulikia malalamiko yanayopokelewa.


Tunaomba vyombo vya habari vitusaidie katika kuhakikisha utaratibu huu mpya unafahamika vizuri kwa umma na kuwahamasisha wananchi wautumie kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu masuala ya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

Jinsi ya kuwasilisha lalamiko kwa simu ya kiganjani:
·         Tuma lalamiko lako ukianzia na neno 'REPORT' kwenda Na0754 460 259. Mfano: REPORT shule ya Msingi Kwetumbali, DSM tunachapwa viboko zaidi ya kumi.


·         Utapokea ujumbe usemao lalamiko lako limepokelewa Tume, na utaelekezwa kama unayo maelezo zaidi yatume kupitia barua pepe: chragg@chragg.go.tz au simu Na. 22 2135747/8.

·         Maafisa wa Tume wanaweza kukupigia simu ili kupata maelezo zaidi kabla ya kuanza kushughulikia lalamiko lako.

·         Lalamiko lako litakapoanza kushughulikiwa, utapata ujumbe wa simu kukujulisha Namba  ambayo utaitumia kufuatilia lalamiko lako. Namba hii itatumwa kwako kupitia namba ya simu uliyotumia kuwasilisha lalamiko lako.

·         Utaweza kujua hatua ambazo maafisa wa Tume wamefikia kwa kutuma ujumbe wa simu pamoja na Namba ambayo utakuwa umepewa baada ya lalamiko lako kufunguliwa jalada.

Jinsi ya kufuatilia lalamiko lako:
·         Tuma ujumbe wako ukianza na neno 'STATUS' kwenda Na.0754 460 259. Mfano: STATUS 13024.

Utaratibu huu wa upokeaji wa taarifa na malalamiko kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani umefadhiliwa na Programu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa nchi zinazoendelea (SPIDER) ya nchini Sweeden (au Swedish Program for ICT in Developing Regions).


Tunaomba ieleweke kuwa utaratibu huu mpya haubadilishi taratibu zilizokuwa zikitumika awali za kuwasilisha malalamiko Tume. Sambamba na uwasilishaji wa malalamiko kwa ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani, Tume itaendelea kupokea malalamiko ya wananchi kwa mlalamikaji kuja mwenyewe kwenye ofisi zetu na kufungua lalamiko lake, na kwa kuandika na kutuma barua kwa njia ya posta, barua pepe au nukushi (faksi.


THBUB ni taasisi huru ya Serikali iliyoanzishwa kama taasisi ya kitaifa iliyo kitovu cha kukuza na kulinda haki za binadamu na wajibu na misingi ya utawala bora.  Ilianzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 chini ya Ibara ya 129 (1) na Sheria Na. 7 ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Mwaka 2001 na ilianza kazi rasmi tarehe 1 Julai, 2001.Tume ina majukumu mengi, baadhi ya majukumu hayo ni:  Kupokea na kuchunguza malalamiko yanayohusu uvunjwaji wa haki  za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na kutoa mapendekezo, kufanya utafiti na kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya haki za binadamu na utawala bora, na kutoa mapendekezo kwa ajili ya kuboresha sheria na kanuni zilizopo au miswada ya sheria na kanuni au taratibu za kiutawala ili kuhakikisha kuwa haki za binadamu na utawala bora vinazingatiwa.


Tume inafanya kazi Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar. Kwa hivi sasa ina ofisi nne (4) zilizoko Dar es Salaam, Zanzibar, Lindi na Mwanza.Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Afisa Uchunguzi Mkuu, Bwana Germanus Joseph
Simu: +255 22 2135222/ 754 768 346.

Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa,
Bwana Wilfred Warioba
Simu: +255 22 2135747/8; 714 818 177.

Saturday, July 20, 2013

SERIKALI YA TANZANIA YASEMA INAFANYA MCHAKATO WA SHERIA YA KUPAMBANA NA UHALIFU KWENYE MITANDAOSerikali ya Tanzania imesema sheria ya kupambana na uhalifu kwenye mitandao iko kwenye mchakato.

Waziri wa Mawasiliano ,Sayansi na Teknolojia wa Tanzania Profesa Makame Mbarawa amesema hivi karibuni jijini Dar es salaam kuwa sheria hiyo itakuwa imekamilika ili kukupambana na uhalifu  kwenye mitandao mbalimbali.

Akizungumza katika mkutano maalum wa kuangalia changamoto na hatua mbalimbali za kimaendeleo katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa nchi zilizo katika ukanda wa Bonde la Ufa uliofanyika jijini Dar es salaam,Waziri huyo amesema Mamlaka ya Mawasiliano  Tanzania imeanzisha kitengo maalum ambacho kazi yake ni kupambana na uhalifu wa mitandao.

Amesema kama kutakuwa na uhalifu umetokea katika nchi jirani basi wananchi watapewa taarifa ili wachukue tahadhari.
Naye  Kamishna wa miundo mbinu na Nishati kutoka Umoja wa Afrika (AU),Dk.Elham Mahmod Ibrahim  aliyekuwa amehudhuria mkutano huo aliwatahadharisha na kuwataka mawaziri wa ukanda wa bonde la Ufa waliohuduhuria mkutano huo kuwa wakali katika kuhakikisha sheria zilizowekwa katika kupambana na wahalifu wa mitandao zinafuatwa na kuchukua mkondo wake.

Friday, July 19, 2013

WATUMIAJI WA INTANETI TANZANIA WAFIKIA MILIONI 5.9


Idadi ya watu wanaotumia huduma ya mtandao wa Intaneti nchini Tanzania imeongezeka kutoka watu 26,000 mwaka 2000 hadi kufikia watu milioni 5.9 Juni mwaka jana.
 
Ofisa wa Idara ya Maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Teknohama) wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania( TCRA) Connie Francis amesema hayo wakati wa semina ya wadau wa mtandao wa Intaneti iliyohusisha uundaji wa kamati ya mpito ya uanzishwaji wa Kituo cha ‘Mbeya Internet Exchange Point’.
Amesema kutokana na umuhimu wa huduma ya intaneti kwa shughuli mbalimbali, idadi ya watumiaji wa huduma hiyo nchini imeongezeka kutoka watu 26,000 mwaka 2000 hadi kufikia watu milioni 5.9 mwaka jana.
Alisema huduma hiyo imerahisisha utoaji wa huduma mbalimbali za kibiashara, kiuchumi na kijamii.
Francis amesema kuwa baada ya kuonekana umuhimu wa huduma hiyo TCRA imeamua kuanzisha mradi ambao utamsaidia mtumiaji kupata huduma hiyo kwa ubora, urahisi na haraka zaidi na kwa gharama nafuu.
Amesema katika kituo hicho watoa huduma wataweza kuweka vifaa vyao na kupata fursa ya kuungana na kurahisisha maendeleo ya mtandao wa Intaneti na kwamba itaisaidia nchi kudhibiti mawasiliano ya ndani na kubaki ndani ya nchi badala ya kutoka nje ya nchi na kurudi ndani.
“Mfumo uliopo kwa sasa ni pale mtumiaji wa mtandao wa Intaneti mawasiliano yake kwenda nje ya nchi ya Tanzania na kurudi hapa kwetu na ndipo baadae kuja kumfikia mhusika. Ni mfumo unaochukua muda mrefu na gharama kubwa kutokana na mzunguko uliopo’’ amesema.
Tayari kamati ya mpito ya uanzishwaji wa kituo hicho imeundwa ambapo imeshirikisha wadau wa mtandao wa Intaneti na itakabidhiwa ofisi pamoja na vifaa hivyo kwa ajili ya kuanza kazi ya kusimamia mfumo huo mpya na kuhamasisha watoa huduma ya mtandao wa Intaneti kujiunga na kituo hicho kwa ajili ya kufanya kazi kwa ufanisi.
Chanzo:Gazeti la Mwananchi

Thursday, July 18, 2013

HIVI NDIVYO FACEBOOK INAVYOPATA PESA KUPITIA KWAKOKuwa na Akaunti ya Facebook ni kwa manufaa yako na manufaa ya Facebook

Facebook ambayo kwa sasa inapatikana katika lugha 70 ulimwenguni, ni mtandao wa jamii ambao unaongoza kwa kuwa na watumiaji wengi zaidi duniani. Wewe na mie kama watumiaji wa Facebook tunainufaisha kampuni hiyo ya Facebook, kwani kupitia kuitumia kwetu kunaiwezesha Facebook kuingiza mapato kwa njia ya moja kwa moja au nyingine.

Makala hii inakuchambulia namna ambavyo Facebook inaingiza "vijisenti" vyake:-1. Kupitia Matangazo: Kwakuwa inao watumiaji wa mtandao wengi, ni rahisi kwa Facebook kushawishi watu binafsi na makampuni kutangaza bidhaa zao kupitia aina mbalimbali za matangazo yanayorushwa hewani na Facebook. Mfano , kampuni inaweza kudhamini POST yake, ili ionekane kwa watu wengi zaidi na mara nyingi. Pia kuna matangazo ya biashara ambapo unaweza kutengeneza tangazo lako la biashara na kulirusha hewani kupitia Ukurasa wako wa Facebook (Facebook Page).  Ili kutengeneza tangazo Facebook, unaweza kuenda sehemu maalum ukiwa Facebook imeandika 
CREATE AN AD.Unahitaji kuwa na Credit Card au Umejisajili na unayo akaunti ya Paypal ili kuweza kulipia huduma hii.Mfano wa Matangazo yanayoipatia fedha facebook
 
 


2. Salio maalum la Facebook ( Facebook Credit)

Ni kama vile unavyonunua salio la simu yako ili utumie salio hilo kupiga simu, ila kwa Facebook, unaponunua Facebook Credit, ni kwa ajili ya kuweza kutumia credit hiyo kulipia kucheza Games, au hata kununua vitu katika baadhi ya maduka yanayouza bidhaa zao ndani ya Facebook.

Unahitaji kuwa na Credit Card au Umejisajili na unayo akaunti ya Paypal ili kuweza kununua Facebook Credit.


3. Kupitia Kuuza bidhaa mbalimbali

Facebook inayo huduma ya kuuza bidhaa mbalimbali kwa mtindo wa "Gift" ambapo wewe mtumiaji unachagua nani unataka kumnunulia bidhaa , kisha unaenda kwa profile ya huyo unayetaka kumuuzia bidhaa. Utaona sehemu imeandikwa GIVE GIFT, ukibofya hapo utakutana na aina mbalimbali za zawadi na maelekezo. Hata hivyo huduma hii ya kutoa zawadi kwa watu haipataki kwa kila nchi. Inabidi ucheki Profile ya mtu husika unayetaka kumpa zawadi kuona kama GIVE GIFT ipo katika profile yake.