OnlineFriday, April 26, 2013

UNAVYOWEZA KUJILINDA NA PACHIKO AMA PICHA USIZOZIHITAJI KWENYE FACEBOOK ANGALIA HAPA


Kumekuwa na changamoto ya kujilinda na watu ambao wanaweza kukuwekea maelezo ama kukutagg picha usiyoihitaji kwenye timeline yako kwenye facebook iwe ni picha ama ni taarifa mbaya ama usizozihitaji.Na utagundua ya kwamba kuna watu ambao hata huwezi amini kama kweli wao wameweka picha zilizo kinyume na maadili na hii imekuwa ikiwakera wao ama watu wanaowasiliana nao kwenye mtandao wa facebook.

Kama inavyoonekana katika picha hapo juu ukifuata hatua hizo itakusaidia kujilinda kwanza ingia kwa timeline yako kulia mwa ukurasa ama timeline yako kuna kialama kinaonekana kama nyota ukishusha chini kasa yako ya mouse unaenda mahali pameandikwa privacy setting bofya hapo na utatokea ukurasa ambao kushoto kuna maelezo bofya palipo andika Timeline and Tagging.

Baada ya hapo utatokea ukurasa mwingine kulia kwake kuna maandishi meusi yameandikwa who can add things to my timeline hapo kuna mahali pa kuchagua Friends ama Only Me,kama ni friends ina maana rafiki yako yeyote anaweza kukuwekea jambo kwenye timeline yako maana hujaizuia,kama ni only me ina maana wewe tu ndo unayeweza kuweka jambo kwa hiyo utaamua angalia kielelezo namba tatu.

Pia kuna mahali pameandikwa Review Posts friends before they appear on your timeline hapo kuna Enable na Disable hapo utachagua enable maana yake uone kwanza wewe ndo itokea kwenye timeline yako vinginevyo utachagua disable kila rafiki yako aweza weka jambo kwenye timeline yako bila wewe kujua kama wewe huja login.

Hatua nyingine ni suala la kujilinda na picha usizozihitaji zitokee kwenye timeline yako kama mtu amekutagg hatua ni zile zile za mwanzo baada ya kuingia kwenye ukurasa wa privacy setting kuna mahali pameandika timeline and tagging  angalia kielelezo namba nne hapo kuna Enable na Disable  hiyo nayo inafanyakazi sawa sawa na pachiko hata kama hujalogin,fuatilia vilelezo vya picha kama zinavyoonekana juu.


Kumbuka baada ya kuweka setting hizi facebook watakuwa wanakutumia ujumbe kwa anuani yako ya barua pepe na kwenye timeline yako ukiwa na picha ama maelezo(jambo)ambalo limetumwa kuonekana kwenye timeline yako wewe utaliona kwanza ndo utaamua hiyo picha ama jambo lionekane kwanye timeline yako,pia unaweza hata kujiondoa kwenye hiyo tagg.


Wednesday, April 24, 2013

TUWE MAKINI NA MATUMIZI YA MITANDAO JAMII


 
 

Mitandao ya kijamii ni mingi sana,ingawa facebook umekuwa maarufu pengine kuliko hata baadhi ya vituo vya redio ama televisheni.
Kwa sasa maelfu ya watanzania zaidi vijana wamejiunga na wanafurahia mawasiliano haya ambayo yameufanya ulimwengu kuwa kweli kijiji.

Ni kawaida sasa kujua anachofanya ndugu yako anayeishi Uingereza,Korea au Marekani ambako tumepishana kwa saa nyingi.Swali la msingi ni kuwa pamoja na raha hii inayotuweka karibu,unaitumia facebook kwa usalama na kwa manufaa?


Unadhani taarifa zako ulizoziweka hazina athari kwako?Tafakari kwa makini,iwapo hisia unazozitoa mara kwa mara zinachukuliwa na hata kueleweka kwa watu wengine,hapana shaka siku hizi facebook imekuwa kama kimbilio au beseni la kuzimwaga hisia za moyoni.

Utamkuta mtu anaandika kwa mfano "Nipo Zanzibar Francoroso hotel na my love'Unadhani ni sawa kila mtu kujua ratiba zako na mpenzi wako?Kuna manufaa yapi kwa umma na marafiki zako wote kujua ulipo na upo na nani?Unadhani marafiki zako hao pengine 300 wanakuwazia mema?
Wengine hutuma picha wakiwa nusu uchi na wanaposifiwa na marafiki zao kuwa wamependeza huona fahari na kumbe wanajidhihaki.

Mtandao huu ni mzuri endapo utatumiwa vyema,lakini napata shaka kuwa watumiaji wake wamejisahau kiasi cha kuyaweka maisha yao yote katika facebook.
Wapo wengi wanaofikia hatua ya kutoa siri zao ambazo ni vigumu kuzisema wazi hata mbele ya marafiki zao.
Ubora wa facebook ni mkubwa lakini pasipo umakini,yapo pia madhara makubwa.

Fumanizi nyingi zimetokea kupitia mitandao hii,talaka,mauaji na hata utekaji vimeshawahi kutokea kupitia facebook,Upo uhusiano uliovunjika tu baada ya mpenzi kubadilisha hadhi yake kutoka ya kuwa na mwenza kwenda single.Uelewa mdogo kuhusu ubinafsi au usiri wa taarifa zetu ndicho chanzo cha kujianika kiasi hiki katika mitandao hii.

Katika maisha haya ya leo,ambayo ni vigumu binadamu kuwajua adui zake ni vyema tukawa makini,wapo ambao huweka taarifa zao zote kuanzia tarehe ya kuzaliwa mwaka na mwezi,hii ni hatari kwani ni rahisi kwa watu wenye nia mbaya kukufanyia lolote au kutumia taarifa zako hata kukuibia.

Kuna kitu kingine nadhani watu hawafahamu kama kina madhara.Matukio na sehemu ulizotembelea kwa kipindi fulani kuonekana kwenye facebook katika eneo la tukio na mahali,Akaunti yako itaonesha mwezi uliopita ulitembelea maeneo na mambo kama hayo.

Inasikitisha kuwa mitazamo mingi ya watu imebadilika kutokana na matumizi ya facebook.Kwa kifupi,watu wanashindwa kujidhibiti.Ni rahisi kufuatilia mawasiliano kati ya watu wawili katika facebook na kujua iwapo kuna uhusiano wowote.

Utafiti mpya umebaini kuwa kati ya watumiaji 300 wa facebook,asiliamia19 hufuatilia tabia za wenza wao.Katika utafiti mwingine ilibainika kuwa watumiaji 1,000,asilimia 25 walivunja uhusiano kwa sababu ya facebook

Wapo wafanyakazi katika taasisi za dini waliojifanya watakatifu,wakatumia facebook kutuma picha wakinywa pombe wakafukuzwa kazi,wengine walimu halafu wanatuma picha wakiwa wanakunywa pombe au wamekumbatiana na wenza,hii inaharibu heshima kwa wanafunzi wako.Mitandao yote ya kijamii ina mengi mema,lakini tuwe makini na namna tunavyoitumia isitiathiri.
Na Florence Majani

Friday, April 19, 2013

TCRA YATOA UFAFANUZI KUHUSU LAINI ZA SIMU ZISIZOSAJILIWA

Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) kupitia Mkurugenzi wake Mkuu Profesa John Nkoma imesema namba za simu zilizosajiliwa nchini humo ni asilimia 93 na asilimia 7 hazijasajiliwa na kwamba asilimia iliyobaki inatakiwa kuondoka.

Akizungumza na wadau wa mawasiliano jijini Dar es salaam jana Mkurungenzi huyo amesema kuwa namba za simu lazima zisajiliwe kwa mujibu wa sheria ya Mawasiliano ya Elekroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010.

Amesema kisheria mtu anayetumia simu isiyosajiliwa akikamatwa anaweza kutozwa faini ya shilingi 50,000 za kitanzania ama kwenda jela miezi sita.

Katika vikao vya pamoja vilivyofanyika Aprili 4 na Aprili 11 mwaka huu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na kampuni zinazotoa huduma za simu za mkononi,zimekubaliana kuchukua hatua za kumaliza tatizo la usajili wa namba za simu na utaratibu wa kufungia namba zote ambazo hazikusajiliwa.

Profesa Nkoma amesema kuwa kwa kushirikiana na  kampuni za simu na vyombo vya usalama imeanza kampeni endelevu ili kuwabaini wanaohusika na uvunjifu wa sheria kwa lengo la kuwalinda watumiaji wema.

Tuesday, April 16, 2013

SERIKALI YA TANZANIA YASEMA:KUTOA TAARIFA ZA SIRI KATIKA MAWASILIANO YA ELEKTRONIKI NI KOSA LA JINAI

                 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Jana na leo, Serikali ya Tanzania imeona kuzuka kwa tabia ya uvunjaji wa kanuni ya utunzaji wa siri za taarifa za mawasiliano binafsi ya watumiaji wa huduma za simu za mkononi. Taarifa hizo zimefikia hatua ya kuchapishwa katika vyombo vya habari kwa kutaja bila idhini yao, namba za simu, wahusika wa namba hizo, maongezi na muda wa mawasiliano Kati yao. Jambo hili ni Kosa la Jinai. Mfano; tamko la Chadema lililotolewa na Ndugu Mabare Marando Mjini Dar es Salaam tarehe 14/04/2013.

Serikali inapenda kuchukua fursa hii kuwakumbusha wenye makampuni ya Simu, Vyombo vya Habari na wananchi kwa ujumla kuwa, kutoa taarifa za mawasiliano binafsi ya simu baina ya watumiaji wa huduma hiyo, ni uvunjaji wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Na. 3 ya mwaka 2010 na Kanuni za Mawasiliano (Kulinda Wateja) za mwaka 2005.

Kifungu cha 98 ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta kinasema;

“Mtu yeyote ambaye ni mfanyakazi wa kampuni yenye leseni ya kutoa huduma za mawasiliano, au mwakilishi wake, ana wajibu wa kutunza siri za mawasiliano binafsi na taarifa zozote za siri za wateja kwa mujibu wa sheria hii”. Aidha, “Mtu yeyote haruhusiwi kutoa taarifa binafsi za mteja yeyote alizopokea au kusikia kwa mujibu wa sheria hii isipokuwa tu mtu huyo ameruhusiwa kwa mujibu wa sheria”

Kanuni ya 12 ya Kanuni za Mawasiliano za mwaka 2005 za Tanzania (Kulinda Wateja) inasema:-

“Mtoa huduma za Mawasiliano haruhusiwa kuingilia kati, kusikiliza au kutoa taarifa zozote za mazungumzo ya mteja yeyote yaliyopitia kwenye mtandao wa mtoa huduma, isipokuwa kwa ruhusa kulingana na mahitaji maalumu kwa mujibu wa sheria zilizopo”

Hivyo basi wananchi wanapewa tahadhari kuhusu kutafuta au kutaka kupata taarifa za mawasiliano ya siri kutoka kwa watoa huduma na kuzitumia taarifa hizo binafsi za mawasiliano pasipo kufuata utaratibu ulioruhusiwa kisheria.

Aidha Serikali inapenda kuwatoa wananchi hofu kuwa Mawasiliano yao (maudhui) hayapaswi kuingiliwa kwa kusikilizwa mazungumzo yao au kusomwa meseji zao katika mitandao ya simu. Serikali Kwa kutumia vyombo vyake vya usalama inawahakikishia wananchi kuwa haki zao za faragha katika mawasiliano zinalindwa Kwa Mujibu Wa Sheria Na. 3 ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010 pamoja Na Kanuni zake.

Kwa taarifa ambazo zimechapishwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari hivi karibuni, Mamlaka ya Mawasiliano pamoja na taasisi nyingine husika kwa mujibu wa Sheria ya EPOCA pamoja na Kanuni zake, wanaelekezwa kufanya uchunguzi wa uvunjwaji huo wa sheria na Mamlaka husika zichukue hatua za kisheria kwa yeyote atakayebainika kuvunja sheria hiyo.

Serikali inayakumbusha Makampuni ya simu, Vyombo vya Habari na wananchi kwa ujumla kuhakikisha siri za mazungumzo binafsi ya wateja zinahifadhiwa na hazitolewi kwa yeyote isipokuwa kwa mujibu wa sheria.


Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo Tanzania
16 April 2013

Monday, April 15, 2013

TCRA YASEMA POLISI NDIO WENYE MAMLAKA WAOTUMIA SIMU VIBAYA

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema Jeshi la Polisi nchini ndilo lenye mamlaka ya kuwakamata watu wanaohusika kutuma ujumbe mfupi wa maneno (sms),  kwenye simu zenye uchochezi au utapeli zinazotumwa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya simu za mkononi.
Aidha, TCRA imesema haihusiki kudhibiti meseji hizo na kwamba anayeweza kushughulikia jambo hilo ni polisi.

Hayo yalisemwa na Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA,Victor Nkya, alipozungumza na kuhusiana na utapeli unaoendelea kufanywa na baadhi ya watu kupitia simu za mkononi.

Alisema watu wanaotumia simu za mkononi kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ni sawa na mtu analiyefanya kosa la jinai ambaye anapaswa kushughulikiwa na polisi.


Alifafanua kuwa matapeli hao wanatumia simu kama nyenzo ya utapeli na ni sawa na mtu yoyote anayetua kitu kumdhuru mwingine, hivyo anakuwa amefanya kosa la jinai na anapaswa kushughulikiwa na polisi.

Alisema kwa mtu yeyote aliyewahi kutapeliwa fedha au kitu chochote anapaswa kwenda kituo cha polisi akiwa na namba ya simu iliyomtapeli kupata msaada zaidi.

Nkya aliongeza kuwa jeshi la polisi pekee ndilo litakaloweza kumpata mhusika aliyetapeli kwa njia wanazozifahamu hata kama mtu huyo hakuisajili namba yake.

“Jeshi la polisi likishapata namba hiyo, wenyewe ndiyo wanajua namna gani ya kumbaini mhusika huyo,” alisema Nkya.

Aidha, Nkya alisema makosa kama kumtukana mtu, au kumfanyia kitendo chochote ambacho ni kinyume na maadili, mlalamikaji anapaswa kutoa taarifa katika kituo cha polisi kilicho jirani naye kwa msaada zaidi.

Kumekuwapo na vitendo vya utapeli vinavyoendelea katika mitandao ya simu za mkononi vinavyofanywa na baadhi ya watu wakijidai kuwa na shida, huku wakihitaji fedha kwa kutumia majina ya marafiki au ndugu wa wanaowatapeli. Matapeli hutumia pia majina ya viongozi wakubwa serikalini na wabunge.

Hadi sasa watu kadhaa wamekwisha tapeliwa fedha kwa kutumiwa sms na matapeli hao pasipo kufahamu na pindi wanapopigiwa simu hawapokei.

CHANZO: NIPASHE

Saturday, April 13, 2013

BAADHI YA MAMBO AMBAYO UNATAKIWA KUWA NAYO MAKINI KWENYE FACEBOOK
 
Facebook imekuwa kama Google ya mitandao ya kijamii. kama sasa hivi hauposti status yako basi unapandisha picha au unajibu quiz ya facebook games. Tunaandika vitu vya ndani kabisa vya maisha yetu ambavyo katika maisha halisi hatuwezi kumwambia yoyote. Tunadhani kwamba ili mradi tumeweka  privacy settings zetu sawa sawa basi tupo salama.

tatizo ni kwamba hatujui nani hasa anatuchunguza habari zetu. Akaunti ya rafiki zatu inaweza ikawa hacked baada ya kuweka program ya ajabu ajabu kwenye simu au computer, au labda mjomba wake ndio anatumia account kwa sababu amesahau ku-log out. lakini vile vile ni internet cafe ambapo wabongo wengi tunapapendaKwa usalama wako na wa familia yako, kuna vitu haupaswi kuviandika Facebook. Kamwe. Hivi hapa ni vitu vitano ambavyo inabidi uvitoe au siviandike kwenye Facebook.

1. Tarehe yako ya kuzaliwa yote kamili.
Sote tunapenda kupata Happy birthday notifications kwenye walls zetu. Inatufanya ndani ya moyo tujisikie raha fulani kwamba kuna mtu  amekumbuka birthday yako na amekutumia wishes. Tatizo ni kwamba unapoweka mwaka wako wa kuzaliwa wote, unawapa wezi nafasi ya kupata moja ya taarifa za muhimu zinazohitajika ili kukuibia. Ni muhimu usiweke na kama ukiamua kuweka basi usiandike mwaka wenyewe. Kwanza marafiki zako halisi wanajua tayari.

2. Hali yako ya mahusiano
Uko kwenye mahusiano au la, ni vyema usiutangazie umma. Stalkers watafurahia kujua kwamba kuna single mpya mtaani.Ukibadilisha status yako kuwa single ndio umewawashia taa ya kijani kwamba umerudi sokoni. Kama ulikuwa umeoa ndio utafanya wajue kuwa upo nyumbani peke yako. Cha busara kufanya ni kutokuandika kabisa.
3. Mahali ulipo
Kuna watu wengi wanapenda ile feature ya facebook ya location tagging ambapo unaweza kum-tag mtu/watu kwamba uko wapi. Tatizo ni kwamba umeshawaambia watu kwamba upo likizo mkoa na sio nyumbani kwako. Tena ukiongeza utakaa muda gani basi wezi/majambazi ndio watajua kabisa ni mmuda gani wakavamie kwako. Ushauri wangu ni kwamba usiandike kabisa. Unaweza kuweka picha zako za safari ukisharudi nyumbani.

4. Kwamba upo nyumbani peke yako
Wasichana wengi wa kibongo ndio wanapenda hii. “Nipo nyumbani peke yangu nimeboreka kweli!” “Nipo lonely nyumbani, nipeni ushauri fans wangu” na vitu kama hivyo ndio utavikuta kwa waTZ wa facebook wengi.

Tunaweza tukadhani ni marafiki wetu tu ndio wanaona post zetu, lakini ukweli ni kwamba hatuwezi kujua nani anasoma tarifa zetu. Mtu anaweza kuiba akaunti ya rafiki yako mradi apate mwanya wa taarifa zako! Unaweza ukaweka privacy settings  lakini kama account ya rafiki yako  ikichezewa, kila kitu kipo wazi.

5.Picha za wanao na tags za majina yao
Wenye watoto mnapenda watoto wenu.Mtafanya chochote kuwalinda na kuwaweka salama. lakini wengi huweka picha za wanao ndani ya facebook na wengine huenda mbali mpaka kuweka picha za wanao kama profile picha!
Wazazi 9 kati ya 10 wameshawahi kuweka picha za wanao na majina yao na wengine kuwa-tag na ndugu, marafiki, na jamaa zao. Taarifa kama hizi zinaweza kutumiwa na wahuni kukuumiza wewe. Wanaweza kutumia jina la mwanao na la ndugu kujenga uaminifu na kumshawishi mwanao kuamini kwamba wao sio watu wabaya au wageni kwenye maisha yake kwa sababu “ona mpaka najua ndugu zako wote na marafiki zako mpaka mama yako na baba yako nawajua!”
Kama kuna haja ya kuweka picha zao basi usiandike majina yao kamili na tarehe zao za kuzaliwa. marafiki zako wa kweli hata hivyo si wanamjua mwanao tayari?
Najua wazazi wengi wanajivunia watoto wao na wanatamani dunia nzima wajue kuwa wanawapenda wanao. Lakini “Kama kweli unampenda, utamlinda”.
Chanzo:tanganyikanblog

UKWELI KUHUSU FACEBOOK HOME KATIKA SIMU ZA ANDROID

Facebook Home
 Facebook wametangaza kitu kipya kwa simu za Android walichokipa jina la Home. Kwa muda mrefu kulikuwa na uvumi kuwa Facebook wanajiandaa kuja na simu yao mpya na hata siku za karibuni ilipotangazwa kutakuwa na tamko toka Facebook uvumi ulisambaa kuwa wanatangaza simu yao mpya lakini haikuwa hivyo.

Mark Zuckerberg, CEO wa Facebook amesema lengo hasa ni kufanya unapowasha simu yako kitu cha kwanza kinachotokea ni watu ulionao Facebook ambapo utatokea ujumbe wa kukufahamisha ujumbe waliokuandikia, maoni na hata tags na utaweza kujibu bila kufungua application yoyote. Yote hii ni kwa ajili ya kuingia katika mfumo wa matangazo kupitia mobile web kwani ni sehemu pekee ambayo Facebook haijaweza kuweka ads zake. 
Android ambayo kwa siku za karibuni imekuwa na watumiaji wengi duniani inaonekana kuwa sehemu pekee ambayo Facebook inaweza kuanzisha utaratibu wa matangazo kwa gharama nafuu kulinganisha na kama wangeamua kuja na simu zao wenyewe.

Layers

Nini Utaweza Kufanya
Pamoja na kuwa na uwezo wa kusoma kila kinachoendelea kwenye account yako ya Facebook pale unapowasha simu, utaweza pia kutuma message wakati ukiendelea kutumia program tumishi nyingine kama Whatsapp au Keek kwa kutumia kitu kilichopewa jina la “Chat Heads”. Ikitokea ukapata message kwa mfano wakati unatumia Instagram, picha ya aliekuandikia itatokeza kwa juu na utaweza kujibu kwa kubofya bila kuacha ulichokuwa unakifanya.


App Launcher

Utaipataje?
App hii imeanza kupatika katika Google Play Store kuanzia April 12. Kama tayari unayo Facebook Messenger au Facebook tumishi yoyote utaombwa uijaribu Home. Ukishaiweka na kuanza kuitumia utagundua kitu kinachoitwa “Chat Heads” ambayo inachukua nafasi ya Facebook Messenger.
Simu Gani Zitakuwa Nayo:

Facebook Home on select phones

Simu zitakazoanza nayo ni HTC One, HTC One X, HTC One X+, Samsung Galaxy S3, Samsung Galaxy S4, na Samsung Galaxy Note II. Simu nyingine zitaongezwa baadae.
Ili kuondokana na usumbufu wa kuiweka kwa kuipakua kwenye Google Store, simu zitakazoanza kutengenezwa baadae zitakuwa zinayo Home moja kwa moja na kwa kuanza HTC watakuwa wa mwanzo kuiweka Home katika simu zao zinazotoka hivi karibuni.Chanzo:Tanganyikanblog

Friday, April 12, 2013

WATUMIAJI WA SIMU NA INTANETI WAONGEZEKA DUNIANI

Takwimu zilizotolewa na Taasis inayosimamia masuala ya mawasiliano ya Shirika la Umoja wa Mataifa Duniani (ITU) 
Februari ,2013 iliyopo Geneva,Uswisi kupitia kituo chache cha kukusanya takwimu za mawasilliano ya teknolojia ya habari na mawasiliano duniani zinaonesha kuwa watu wanaotumia wa mawasiliano ya simu wamefikia bilioni 6.8 kati ya watu bilioni 7.1 waliopo duniani.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa matumizi ya simu za mkononi yameongezeka kwa asilimia 96 duniani ambapo asilimia 128 katika nchi zilizoendelea na kwa nchi zinazoendelea ni asilimia 89.

Kwa upande wa mawasiliano ya intaneti watu bilioni 2.7 duniani ambao ni karibia asilimia 40 ndio waliounganishwa katika matumizi ya mawasiliano hayo ambapo wanawake ni asilimia 16 tu.

Katika nchi zinazoendelea asilimia 31 wameunganishwa kwenye mitandao ya komputa ukilinganisha na asilimia 77 ya watu wanaotoka katika nchi zilizoendelea.Ambapo matumizi ya interneti barani Ulaya ni asilimia 75 na nchi za bara la Amerika ni asilimia 65,wakati barani Afrika ni asilimia 16 tu.

Takwimu hizi zinaonesha kuwa kumekuwa na kiwango kikubwa cha matumizi ya intaneti kwa wanaume kuliko wanawake duniani  kwani ni asilimia 37 tu ya wanawake wanaweza kuwa katika mitandao ambapo wanaume ni asilimia 41.

Katika nchi zinazoendelea kuna wanawake milioni 826 wanaotumia intaneti na wanaume ni milioni  980 na katika nchi zilizoendelea wanawake wanaotumia inteneti ni milioni  475 ambapo wanaume ni milioni 483.Ambapo inaonekana kuna tofauti ya asilimia 16 kati ya wanaume na wanawake katika matumizi ya teknolojia hiyo ya mawasiliano katika nchi zinazoendelea na katika nchi zilizoendelea ni tofauti ya asilimia 2 tu.

Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa inakadiliwa kuwa  kufikia mwishoni mwa mwaka 2013 jumla ya kaya 750 ambazo ni sawa na asilimia 41 duniani ndizo ambazo zitakuwa zimeunganishwa na mawasiliano ya intaneti.

TAARIFA YA TCRA KUHUSU UUZAJI, USAJILI NA MATUMIZI YA LAINI ZA SIMU ZA MIKONONI


MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
 
TAARIFA KWA UMMA
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni chombo cha Serikali
kinachosimamia masuala ya mawasiiliano Tanzania. Mamlaka ilianzishwa kwasheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na. 12 ya mwaka 2003 kusimamia Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.
 
Mwaka 2010, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria la Mawasiliano ya Elektroniki na Posta (EPOCA) kusimamia, pamoja na mambo mengine, uuzaji, usajili na matumizi ya laini za simu za mkononi, ambazo kwa kiingereza zinaitwa “
Subscriber Identification Module”, na kwa kifupi SIM, katika Jamhuri ya Muungano waTanzania. 
 
Mamlaka inapenda kuwakumbusha wananchi kwa ujumla kwamba sheria hiyo imeainisha makosa yanayotokana na kukiuka vipengele vya sheria iliyotajwa hapo juu. 
 
Makosa hayo ni kama ifuatavyo:
a)Kuuza au kusambaza laini ya simu bila kibali cha mtoa huduma za simu
ambaye ana leseni kutoka TCRA;
b)Kutumia laini ya simu ambayo haikusajiliwa;
c)Kutoandikisha taarifa za laini husika kabla ya kuitoa au kuiuza;
d)Kutoa taarifa ya uwongo au maelezo yasiyo sahihi wakati wa kusajili laini
ya simu;
e)Kuchakachua simu ya mkononi au laini ya simu;
Mamlaka inawakumbusha watoa huduma wote na wakala wao kwamba ni wajibu 
 
wao kuzingatia yafuatayo:
a)Kuweka kumbukumbu na taarifa kuhusu wakala
wao wanaouza laini zao za simu;
b)Kuandikisha watumiaji wanaonunua au kupatiwa
laini za simu;
c)Kuhakiki taarifa zinazotolewa waka
ti wa usajili wa laini za simu;
d)Kuhifadhi nakala ya vitambulisho au nyaraka zozote zilizotumika wakati wa
kusajili laini husika ya simu;
e)Kutokutoa taarifa za wateja bila idhini ya Mamlaka husika;
f)Wauzaji wa laini za simu walioidhinishwa wana wajibu wa kuwasilisha
taarifa za wateja kwa watoa huduma;
g)Wauzaji wa laini za simu walioidhinishwa wana wajibu pia wa kutokuuza
laini za simu bila idhini ya Mtoa Huduma;
Kama ilivyoanishwa kwenye sheria ya EPOCA ya mwaka 2010 na Kanuni za
Sheria hiyo za mwaka 2011,masharti ya usajili wa laini za simu ni kama
ifuatavyo: 
 
1.Mtoa huduma au wakala analazimika kujaza fomu ya usajili;
2.Mteja Mtarajiwa anatakiwa kuonyesha mojawapo ya vitambulisho halisi
vyenye picha yake;
•Pasipoti
•Kitambulisho cha kazini
•Leseni ya udereva
•Kadi ya usajili wa Mpiga Kura
•Barua ya utambulisho kutoka Se
rikali za Mitaa ikiwa na picha
•Kitambulisho cha Taifa
•Kitambulisho cha SACCOs
•Kadi ya benki yenye picha
3.Watoa huduma wanatakiwa kuhifadhi ukurasa wa kwanza wa fomu ya usajili;
4.Mteja anatakiwa kupatiwa nakala ya fomu au hati itakayothibitisha kwamba amejisajili;
5.Mtoa huduma au Wakala atabakia na nakala ya kitambulisho 
 
Wateja waliojiandik isha wanaweza kuhakiki usajili wao kwa kupiga *106#.
Mtu yeyote ambaye atakiuka vipengele vya Sheria ya EPOCA ya mwaka 2010 na
kupatikana na hatia kwa mujibu wa vifungu vya Sheria hiyo ataadhibiwa kwa
kutozwa faini au kufungwa jela au vyote kwa pamoja. 
 
Imetolewa na
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
Mawasiliano Towers
Namba 20, Barabara ya Sam Nujoma Road
S.L.P. 474
14414 Dar es Salaam

Monday, April 8, 2013

WANAOTUMIA VIBAYA MITANDAO JAMII NA SIMU KUCHUKULIWA HATUA KALI

Serikali ya Tanzania imesema itawachukulia hatua kali za kisheria kwa mtu yeyote atakayebainika kutumia vibaya simu za mikononi na mitandao ya kijamii kuleta uchochezi au kwenda kinyume na maadili ya nchi hiyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mwishoni mwa juma Waziri wa Sayansi na Teknolojia,Makame Mbarawa amesema lengo la kufanya hivyo ni kukomesha vitendo vya hatarai vinavyoonekana kukua siku hadi siku nchini Tanzania.

Amesema hatua zitachukuliwa dhidi ya kampuni au mtu yeyote atakayetumia njia hizo za mawasiliano kutoa kashfa ama kuitukana serikali,viongozi wa serikali,dini,siasa na watu binafsi kwa kuwa vitendo hivyo vinakiuka sheria za nchini.

Hatua hizo za serikali pia zitawahusu watu wote wanaojihusisha na uonyeshaji kwenye mitandao hiyo picha za ngono,unyanyasaji wa watoto na ukiukwaji wa maadili na kutoa taarifa zenye lengo la kuvunja utulivu na amani.

Teknolojia ya habari na mawasiliano katika miaka ya hivi karibuni imechangia kuleta maendeleo nchini Tanzania lakini baadhi ya watu wanaitumia kwa mambo yasiyofaa  ikiwa ni pamoja na wizi,ujambazi,ubakaji,biashara ya dawa za kulevya, ukahaba na kusambaza siri za watu binafsi bila idhini ya wahusika.

Friday, April 5, 2013

VISIMBUZI VYASITISHWA KWA MUDA NCHINI TANZANIA

Wizara ya Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania imeamua kusitisha awamu ya pili ya kuzima mitambo ya analojia na kuwasha dijitali,ili kufanya tathimini yaliyojiri katika awamu ya kwanza.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia wa Tanzania Profesa Makame Mbarawa amesema hatua hiyo ni ya muda ili kupisha tathimini hiyo.

Profesa Mbarawa alisema serikali haina mpango wa kusitisha kuwasha mitambo ya dijitali na kuzima ya analojia bali inachofanya sasa ni kuhakikisha mchakato mzima wa dijitali unafanikiwa nchini.

Awamu ya kwanza ya uzimaji wa mitambo ya analojia ilihusisha mikoa saba ikiwemo mikoa ya Dar es salaam,Tanga,Dodoma,Mwanza,Arusha na Mbeya inayotarajiwa kuzimwa rasmi mitambo yake mwishoni mwa mwezi huu.

Awamu ya pili inayotarajiwa kuanza wakati wowote na kuhusisha mikoa zaidi ya 14,wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau na kamati za Bunge ya Miundombinu walikubaliana kwa kuda hadi tathmini ya kina itakapofanyika katika mikoa saba iliyoanza kutumia mfumo mpya wa dijitali.

Waziri huyo amesema kuwa msimamo wa serikali kuhusu suala hilo la matumizi ya dijitali ni kuhakikisha kuwa hadi ifikapo juni 17,2015 dunia nzima itazima mitambo ya analojia na kuwasha dijitali na hivyo Tanzania nzima itakuwa tayali inatumia mfumo huo mpya.

Wednesday, April 3, 2013

UFISADI KAMPUNI ZA SIMU NCHINI TANZANIA

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Kudumu za Serikali imebaini madudu yanayofanyika katika uwekezaji wa kampuni za simu nchini Tanzania na kuisababisha serikali kukosa mapato ya shilingi za kitanzania trilioni 1.8 kwa mwaka.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Zitto Kabwe hakuwa tayari kueleza maeneo ambayo Serikali imekuwa ikipunjwa kodi na kampuni hizo na badala yake amesema wameunda kamati ndogo ya watu watatu kwa ajili ya kuchunguza wizi huo.

Kamati hiyo ilibaini madudu hayo baada ya kukutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Mamlaka ya Bandari (TPA) na Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA).

Akizungumza na waandishi wa habari, Zitto alisema wameitaka TRA kuandika mapendekezo ya kufanyiwa marekebisho ya sheria ya fedha ya 2012, ili iwe na uwezo wa kuhakiki uwekezaji wa kampuni za simu na kufanya ukaguzi wa miradi husika ili kubaini kama inafanana na kodi inayotozwa.

Alisema kampuni hizo zina misamaha mikubwa ya kodi ambayo inatolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) bila kushirikisha wadau mbalimbali na kwamba hivi sasa Serikali inapata Sh300 bilioni tu kwa mwaka kama fedha za mapato ya kampuni hizo.

“Misamaha kwa kampuni za mawasiliano ni miaka mitano na TIC inaweza kuongeza miaka mingine mitatu. Kutokana na hali hiyo tunahitaji marekebisho ya sheria ili tuweze kuzibana hizi kampuni ziweze kulipa kodi na kuchangia pato la ndani,” alisema Zitto.

Zitto alisema mbali na mapendekezo hayo, pia wamemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua misamaha yote ya kodi inayotolewa na TIC ili kujiridhisha kabla ya kutoa uamuzi wa kuendelea nayo ama vinginevyo.


 Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema: “Kuna fedha zinakatwa kienyeji tu na kampuni hizi, mfano kwa watu 5 milioni kwa siku wanapata Sh1.8 bilioni, sasa kama kampuni hii itakuwa na wateja zaidi inapata kiasi gani, fedha hizi hazipo katika mlolongo wa ukatwaji wa kodi.

“Pia tutahitaji maelezo ya jinsi mnavyodhibiti meseji za chuki ambazo tunaziona kila siku katika simu zetu, pia kampuni hizi zimekuwa zikibadili majina kila baada ya muda fulani jambo ambalo pia linakosesha nchi mapato.”

TRA na TCRA
Mkurugenzi Mkuu wa TRA, Harry Kitilya alisema kinachowakwamisha ni sheria zilizopo, kwamba wanashindwa kukusanya mapato kwa kuwa kampuni hizo zina misamaha ya kodi.
“Misamaha hii ndiyo inatupa wakati mgumu kukusanya mapato, ila kama sheria hii ya misamaha ya kodi itafanyiwa marekebisho tutaweza kuingia kiasi kikubwa cha kodi,” alisema Kitilya.

Naye Profesa Nkoma alisema ili kuzibana zaidi kampuni za simu kuanzia mwezi Julai mwaka huu utafungwa mtambo maalumu wa kudhibiti mawasiliano (TTMS).
Chanzo:Mwananchi