OnlineThursday, March 28, 2013

MITAMBO YA ANALOJIA MOSHI NA ARUSHA KUZIMWA MACHI 31,2013

 

Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) inatajia kuzima mitambo ya analojia ya kurusha matangazo ya Televisheni na kuwa katika mfumo wa dijitali machi 31,mwaka huu katika mji wa Moshi na jiji la Arusha.

Mhandisi mkuu wa masuala ya utangazaji wa TCRA,Andrew Kisaka akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro juma hili ameyataja maeneo yatakayohusika na zoezi hilo ni Manispaa ya Moshi,Mabungo,Himo,Chekereni,Bomang'ombe na Njia Panda.

Katika hatua nyingine TCRA imetoa taarifa kuwa zaidi ya visimbuzi 50,000 vya Star Times vimeuzwa katika mkoa wa Arusha kabla ya kuzimwa kwa mitambo ya analojia 


TTCL KUTOA HUDUMA YA MAWASILIANO VIJIJINI


 

Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) inatarajia kutoa huduma katika maeneo ya vijijini kwa gharama ya shilingi bilioni tatu na nusu.Taarifa ya ushindi wa zabuni wa kampuni hiyo iliyotolewa leo katika vyombo vya habari inaonesha kuwa TTCL itatoa huduma za mawasiliano katika kata 20 zenye jumla ya vijiji 103 na jumla ya wakazi zaidi ya 160,000 katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Mradi huu ni wa kitaifa wenye lengo la kusaidia maeneo yasiyokuwa na huduma za mawasiliano kwa muda mrefu sasa.Mradi ambao umefadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia kitengo cha kuboresha huduma za mawasiliano vijijini,ambacho kipo chini ya Wizara ya Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia.

Vijijini husika vya mradi huu viko katika mikoa 10 ambayo ni Arusha,Manyara,Dodoma,Lindi,Mbeya,Morogoro,Mtwara,Ruvuma,Shinyanga na Tanga.

Huduma zitakazotolewa katika mradi huu ni simu yaani maongezi,huduma za ujumbe mfupi (sms) na mtandao wa internet zote kwa teknolojia mchanganyiko za mkongo na isiyokuwa na waya.
Monday, March 18, 2013

CHANGAMOTO ZA KUJILINDA KATIKA MITANDAO

 

Miongoni mwa changamoto inayoonekana kwa sasa katika teknolojia ya habari na mawasiliano (Teknohama) ni suala la ulinzi katika mitandao,japo pia baadhi ya wanateknohama hawafahamu sheria na kanuni za kuisalam  zinazotumika katika masuala mbalimbali ya teknohama na hasa katika suala la kujilinda kwa mtumiaji wa mitandao mbalimbali ya internet.

Juma hili yamejitokeza matukio mawili ambayo yaweza kuwa mfano wa kuyatumia katika hili kwanza ni Mama mmoja anaitwa Mama Matinde mkazi wa jijini Dar es salaam ambaye wataalamu wa teknolojia wanaoingilia mifumo mbalimbali ya mawasiliano (hackers) ambao wameingilia anuania yake ya barua pepe bila yeye kufahamu  na kuwasiliana na watu anaowasiliana nao na kuwaambia kuwa yuko safarini nje ya nchi na hivyo kapata matatizo wamtumie pesa wakati si kweli.

Blog hii imezungumza na kwa njia ya simu Mama Matinde na ameeleza kwa sasa yuko Burundi na si katika nchi ambayo mhalifu ameitaja,anasema toka jana  hawezi tena kuingia kwenye email yake na hivyo imebidi atengeneze anuani nyingine ya barua pepe.

Matukio haya yamekuwa yakitumiwa sana na hawa wataalamu wa mifumo ya mawasiliano ya komputa katika kufanikisha uhalifu wa mitandao ili kujipatia fedha kwa udanganyifu fikiria akiwasiliana na rafiki zako 50 akawaambia kila mmoja amtumie 50,000 atakuwa na shilingi ngapi?

Tukio lingine ni taarifa ya Ridhiwani Kikwete ya  machi 17,2013 ambayo imenukuliwa na mtandao jamii wa wanabidii inaeleza  kuwa mojawapo ya mambo makubwa ambayo yamejitokeza siku za karibuni hasa katika suala la Teknolojia na habari ni jambo la sheria za faragha (privacy and privacy laws). 

Ridhiwani anasema tumeshuhudia kufungwa kwa gazeti za News of The World, mali ya bilionea Rupert Murdoch wa Kimarekani baada ya kudhihirika alitumia wataalam wa teknolojia (hackers) kutafuta siri za watu mashuhuri kwa kuingia katika simu zao za mkononi kinyume cha utaratibu na sheria za faragha (Privacy Laws). 

Anaeleza  wahalifu hao hao wa mtandao wamekuwa wakifanya mengi kama kuvamia kwa mitandao ya makampuni makubwa kama Sony na mengineyo na hata katika mitandao hii ya kijamii upo wakati marafiki zako wanakwambia mbona umenitumia kitu kisichoeleweka, na baadaye kuja kugundua kwamba si wewe uliyefanya hivyo.
 

Ridhiwani anasema Tarehe 1, 8 na 9 mwezi huu wa Machi alikuwa Dar es Salaam kwa shughuli zake za kawaida kimaisha lakini ziko updates 5 zilifanyika kwenye wasifu wake wa facebook  moja ikimhusu mwandishi wa habari Absalom Kibanda aliyepigwa na watu wasiojulikana na kujeruhiwa na hivyo kwenda kutibiwa nchini Afrika ya Kusini.

Ridhiwani katika taarifa yake hiyo anasema  tarehe hizo mwezi huu wa Machi, wahalifu wa mtandao wakiwa eneo la Njiro na baadaye Kijenge mjini Arusha (Kila post ilionyesha eneo ilipotoka), (wakati huo yeye akiwa Dar es Salaam) waliingia bila idhini kwa njia haramu (Hacking) katika anuani yake ya  Facebook na ku-post habari hizo tano. 


Kutokana na matukio haya mawili yaani la Mama Matinde na hili la Ridhiwani Kikwete kuna changamoto kubwa sasa kwa watumiaji wa mitandao hasa masuala ya usalama katika mitandao,inashauriwa kuwa neno la siri la kuingilia katika anuani ya barua pepe inatakiwa liwe lenye mchanganyiko wa herufi na namba yaani liwe gumu kwa mtu kulibashiri baadhi huwa tunatumia miaka ya kuzaliwa na hivyo mtu aweza kubahatisha akaaingia bila wewe kujua ana akamua kufanya chochote bila mhusika halisi kujua,pia inashauriwa uwe unabadilisha neno hilo la siri kila baada ya miezi mitatu yaani usitumie neno moja la siri kwa muda mrefu.

Suala lingine ni kuhusu usalama katika mitandao jamii hasa facebook na twitter,skype ambazo zinaonekana kuwa  na watumiaji wengi na zingine zimeunganishwa kwa maana ya kwanza unaweza kuwa na wasifu kwenye mitandao mitatu na unaingia kwa kutumia neno moja la siri ama ukishaingia kwenye mtandao mmoja wa kijamii moja kwa moja utakuwa umeingia kwenye mtandao mwingine kwa hiyo unaweza ukajisahau na mtu akatumia mwanya huo kuingia bila idhini yako.

Baadhi ya watumiaji wa facebook wamekuwa wakijisajili kwenye mtandao huo wa kijamii na kuonesha namba za simu na anuani zao za barua pepe wazi hili nalo sio jambo jema katika kujilinda na wahalifu wa mitandaoni ambao wanaweza kutumia mwanya huo kufanya lolote baya katika wasifu wako na kuonekana umefanya wewe ikiwa ni pamoja na kukuchafua ama kufanya uhalifu na kuonekana wewe ndo umefanya.

Kosa lingine ni kutoweka vizuizi vya faraga katika mitandao jamii ambavyo waundaji wa mitandao jamii wameiweka na kuifafanua lakini wengi wetu hatusomi ama hatuifahamu,juma lililopita wasifu mmoja wa kanisa la waadventista wasabato kwenye mtandao wa kijamii wa facebook mtu mmoja anayetumia jina la kike aliweka picha ya mwanamke akiwa uchi na picha hiyo ikaonekana katika wasifu huo wa kanisa mpaka blog hii ilipowasiliana na msimamizi wa wasifu huo ili kuiondoa picha hiyo chafu.

Bado kuna changamoto nyingine ya kutofahamu kujilinda hasa kwa watu wanaotumia simu za kisasa (smartphones) ambazo zina GPRS mfumo unaofanyakazi kwa simu za kisasa kama kuna mawasiliano ya internet ambayo inaweza kuonesha mahali ulipo kama umeiweka on hasa kama unaweka pachiko ama unawasiliana na mtu kwenye mtandao jamii kama vile facebook.

Bado kunahitajika utoaji wa elimu ya teknohama kwa jamii hasa nchini Tanzania.Kwa maelezo zaidi waweza kuendelea kusikiliza kipindi cha maisha na tekhohama Morning Star Radio kila jumapili saa 3:00 asubuhi.MOROGORO 98.9 FM,MWANZA  102.1FM, MUSOMA 98.9 FM, KIGOMA 103.3 FM,  ARUSHA 102.5 FM, MBEYA 106.9 FM na DAR ES SALAAM   105.3 FM.
  1  

3  
   
 


 

 


 Wednesday, March 13, 2013

BENK KUU YA TANZANIA YAINGILIA KATI WIZI KWA KUTUMIA ATMBenki Kuu ya Tanzania (BoT), imeingilia kati wizi wa fedha kwa kutumia mashine za kutolea fedha (ATM), ambao umeibua hofu kubwa katika sekta ya benki nchini.

Kutokana na wizi huo kukithiri katika baadhi ya benki, wafanyabiashara na wananchi wameanza kujipanga kuondoa fedha zao katika akaunti.


Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu alizungumza kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki kwamba wameziagiza benki kuweka kifaa cha umeme (electronic chip) kwenye kadi zao za ATM ambazo si rahisi kughushi.


“Wizi kama huo unatokea wakati mtu anaweka namba za siri kwenye ATM kwani kuna watu huweka kamera ambazo husoma na namba hizo kufanikiwa kuzipata kisha kufanya wizi ,” alisema Profesa Ndullu.


Alisema kuwa kutokana na wizi kukithiri wamezitaka benki zote kuweka mifuniko katika eneo la namba za siri ili wezi wanaoweka kamera ili kuzinasa wakati mtu anatoa fedha washindwe kufanya hivyo.


Profesa Ndullu alisema wanafuatilia mfumo wa utendaji wa benki ili kuondokana na tatizo hilo ambalo hivi sasa limeibua mijadala na hofu kubwa miongoni mwa wananchi.


Benki kubwa nchini zimekumbwa na mtikisiko wa wizi wa fedha kwa kadi za ATM, ambao umeongezeka kwa kasi kiasi cha kufanya wananchi wengi kuhifadhi fedha zao kwenye mitandao ya makampuni mbalimbali ya simu za mikononi ambayo hata hivyo ripoti zimekuwa zikieleza kuwa nako usalama wake si wa kiwango cha juu.


Baadhi ya benki ambazo zimekumbwa na matukio hayo zimekuwa zikisita kutoa taarifa kueleza sababu za kushindwa kuzuia wizi huo na badala yake zimekaa kimya kuhofia kupoteza wateja.


Kukua kwa teknolojia za kifedha ambako kumerahisisha ufanisi wa matumizi na utunzaji wa fedha, sasa kunaonekana kugeuka na kuwa balaa kutokana na kuibuka kwa wizi mkubwa mahala zinakohifadhiwa kwenye akaunti za wateja kwa kutumia njia ya mtandao.


Taarifa za wizi huo zilianza kurindima mwezi Machi, 2010, ambako kiasi cha mabilioni ziliibwa kupitia katika mashine za ATM huku kati ya kiasi hicho jumla ya Sh360 milioni zikihusisha benki moja nchini.


Hata hivyo, mwaka huo watu wanne walikamatwa baada ya kuripotiwa wizi huo mkubwa. Sambamba na kukamatwa kwa watu hao, pia alikamatwa mfanyabiashara mmoja aliyekuwa akifanya jaribio la kuiba kimafia Sh221 milioni kutoka benki ya NBC.


Wimbi la wizi huo limeibuka tena katika kipindi cha Oktoba 2012 hadi Februari 2013 na inakadiriwa kuwa jumla ya kiasi cha Sh700 milioni kimeibwa katika benki mbalimbali kwa nyakati tofauti.

Chanzo:Gazeti la Mwananchi

WIZARA HAIJAPOKEA MAOMBI YA KUSITISHA MATANGAZO YA TELEVISHENI

Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia  Profesa Makame Mbarawa amesema hajapokea maombi ya Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania nchini Tanzania (MOAT) kuhusu kusitisha kurusha matangazo ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa kutokana na kushindwa kumudu gharama za uendeshaji wanazodai zinatokana na urushaji wa matangazo kwa njia ya dijitali.

Kupitia kipindi cha Radio One asubuhi ya leo,Waziri Mbarawa amesema hajapokea ombi hilo ambalo hafahamu linaeleza nini na atakapolipokea wizara italifanyia kazi japo amesema wamiliki wa vituo vya televisheni nchini walikubaliana na wizara katika uhamishaji wa masafa ya utangazaji kutoka analojia kwenda dijitali mchakato ambao ulianza mwaka 2005  na vyombo hivyo vilikubali kutumia teknolojia hiyo. 

Kabla ya kuanza kwa zoezi la kuzima mitambo ya analojia disemba 31,2012 vyombo vyote vya utangazaji viliitwa na kusaini makubaliano ya kuzima mitambo na kuanza kurusha kwa njia ya dijitali.Nayo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema haitarudi nyuma kwenye suala la kutumia mfumo wa matangazo kupitia njia ya dijitali na kwamba mfumo huo utaendelea kutumika.
 


TCRA ilizima mitambo ya analojia na kuhamia dijitali, Desemba 31, mwaka jana kitendo ambacho Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) wanadai kimepunguza mapato yanayotokana na matangazo.